WIZARA YA AFYA YATOA UFAFANUZI WA CHANJO YA UVIKO-19 KWA WANAOSAFIRI NJE YA NCHI


Dr. Leonard Subi

Na Dotto Kwilasa,Dodoma.
WIZARA ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto kitengo Cha huduma za Kinga imewatoa hofu Watanzania ambao wamepata chanjo ya UVICO-19 na wana dharula ya  kusafiri nje ya Nchi kwa takwa la kuwa na cheti cha kielekroniki kufika kwenye kituo walichopatiwa chanjo ambapo utaratibu wa dharula wa kuhakiki na kuingiza taarifa zake kwenye mfumo utafanywa na kupatiwa cheti.

Pia  imewataka Waganga wakuu wa mikoa nchini kote  kukamilisha zoezi la ujazaji wa taarifa za wateja ambao walipatiwa chanjo kabla ya mfumo kwenye fomu maalumu Kabla au ifikapo tarehe 25 Agosti 2021.

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Dr. Leonard Subi amesema hayo Jijini Dodoma wakati akitolea ufafanuzi juu ya maendeleo ya utoaji wa chanjo ya UVICO-19 Pamoja na vyeti vya chanjo hiyo huku akifafanua Kuwa baada ya kukamilisha zoezi hilo  wahakikishe wanavituma wizarani ili kuwezesha taarifa zao kuingizwa kwenye mfumo ambapo wataweza kupata vyeti vyao kwa njia ya kielekroniki .

Kutokana na hayo amewataka wasimamizi wa zoezi la chanjo ya UVICO-19 kwa ngazi ya mikoa na Halmashauri kuimarisha usimamizi Kwa kuhakiki vyeti ili kuondoa kero na usumbufu.

Dr. Subi ameeleza Kuwa Pamoja na Mafanikio yaliyopo kwa Wananchi wengi kuendelea kujitokeza kupata chanjo ,bado Kuna changamoto ya upatikanaji wa vyeti Kwa wateja huku akisema Kuwa tayari zimeshaanza kushughulikiwa na maelekezo kutolewa kwa Waganga wakuu wa mikoa nchini kote.

"Zoezi la utoaji chanjo linaenda sambamba na utolewaji wa vyeti Kwa wateja ,Katika kufanikisha hili la utolewaji wa vyeti Wizara Kwa kushirikiana na Chuo kikuu Cha Dar  es Salaam  iliandaa mfumo wa kielekroniki ambao unamwezesha mtoa huduma kuingiza taarifa za mteja aliyechanjwa ili aweze kupata cheti,"amesema.

Kadhalika Mkurugenzi huyo mwenye dhamana ya huduma za Kinga,ameelekeza utaratibu wa kupata cheti hicho kuwa,"Kwa mteja aliyefanya booking Kabla, akifika kituoni mhudumu atamtafuta Katika mfumo Kisha atahakiki taarifa zake ,kumpatia chanjo na kisha kupewa cheti kupitia mfumo wa kielekroniki,"amesema.

Aidha ameongeza kuwa mfumo uliopo pia utamtumia mteja ujumbe na linki ya kupata cheti kielekroniki kwenye simu yake ya mkononi baada ya kupata chanjo ambapo anaweza kwenda kuprinti popote.

"Kwa mteja ambaye hakufanya booking kabla,watoa huduma watamsaidia kujisajili kwenye mfumo na kumpatia chanjo kisha atapata cheti cha kielekroniki,"amesema na kuongeza;

"Kwa kuwa mfumo huu unategemea uwepo wa mtandao Katika kituo husika ,Wizara inaelekeza matumizi ya vyeti vya kawaida kuendelea pale ambapo mfumo wa kielekroniki hauwezi kutoa vyeti,kwa kuzingatia hilo hadi Sasa zaidi ya vyeti milioni Moja na laki mbili vimesambazwa Katika mikoa yote ya Tanzania bara,"amefafanua.

Katika hatua nyingine Mratibu wa chanjo Mkoa wa Dodoma Francis Bujiku amesema utaratibu wa utoaji chanjo ya UVICO-19 unaendelea Kupitia vituo 28 vya kutolea huduma za Afya vilivyoidhinishwa Mkoani hapana kwamba hadi Sasa jumla ya watu elfu 12 tayari wameshapatiwa chanjo hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post