WAZIRI NDUMBARO AZINDUA ZOEZI LA UWEKAJI ALAMA KWA FARU ENEO LA HIFADHI YA NGORONGORO.


Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro (wa sita kutoka kushoto) akishuhudia uzinduzi wa zoezi la uwekaji wa alama za utambuzi wa faru katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.


Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas ndumbaro akiongea na menejimenti na wadau wa uhifadhi wa Faru katika eneo la Kreta ya Ngorongoro wakati wa uzinduzi wa zoezi la uwekaji alama za utambuzi kwa mnyama faru.


Mkurugenzi wa Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Maurus Msuha akielezea zoezi la kuweka alama kwa Faru kama sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kimataifa wa kuhakikisha kuwa maeneo yote yanayopatikana faru yanalindwa kwa kuwekewa alama za utambuzi.


Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Freddy Manongi akielezea upekee wa Hifadhi ya Ngorongoro kwa eneo pekee unaloweza kuona faru weusi wakiwa katika maeneo yao ya asili.


Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro (kulia) akimkabidhi cheti Kiongozi wa mradi wa Frankfurt zoological Society Bw. Rian Labuschagne kama ishara ya kutambua mchango wao katika mradi wa uhifadhi wa Faru Nchini.

*****************************

Na Kassim Nyaki-NCAA

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro amezindua zoezi la uwekaji wa alama kwa faru katika hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa Wanyama hao ambao ni zao kubwa la Utalii nchini



Dkt. Ndumbaro ameeleza kuwa Wanyama aina ya faru ni adimu na muhimu sana katika utalii na Uhifadhi hivyo ulinzi wao kwa kutumia teknolojia ya kisasa ni kipaumbele kuwezesha ufuatiliaji wa mienendo yao hasa wanapozunguka maeneo mbalimbali ndani ya Hifadhi.

“Faru ni zao muhimu katika Utalii na Uhifadhi, katika kuimarisha zao hili nawapongeza NCAA kwa hatua hii ya kushirikiana na wadau kubuni mfumo wa teknolojia ya kisasa unaosaidia kulinda na kufuatilia mienendo ya Faru hasa wanapotoka nje ya Hifadhi na kuingia kwenye mashamba ya watu” alisema Dkt. Ndumbaro.

Waziri Dkt. Ndumaro ameongeza kuwa Utalii wa Faru ni zao muhimu katika kuongeza pato la Nchi na idadi kubwa ya wageni wanaokuja Ngorongoro moja ya kivutio kikubwa kwao ni Faru hivyo teknolojia ya kuwalinda faru inasaidia kuongeza idadi yao kwa haraka zaidi.

Mkurugenzi wa Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Maurus Msuha ameeleza kuwa zoezi la kuweka alama kwa Faru ni utekelezaji wa mpango wa kimataifa wa kuhakikisha kuwa maeneo yote yanayopatikana faru yanalindwa kwa mbinu za kisasa na faru hao kuwekewa alama za utambuzi ili kuwafuatilia mienendo yao kwa urahisi zaidi.

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Freddy Manongi amebainisha kuwa Hifadhi ya Ngorongoro ndio eneo pekee Tanzania na duniani kote ambako mtalii anaweza kuwaona faru weusi wakiwa katika maeneo yao ya asili.

Ameahidi kuwa NCAA itaendelea kuhakikisha kuwa wanatumia mbinu zote za kisasa kuwalinda na kuwahifadhi faru hao ili waweze kuishi kwa mda mrefu zaidi kama ilivyokuwa kwa faru mkongwe zaidi ambaye alikufa katika hifadhi ya Ngorongoro mwaka 2019 akiwa na umri wa miaka 57.

Kiongozi wa mradi wa wa Frankfurt zoological Society Bw. Riam Labuschagne ambao ni wadau muhimu katika Miradi ya uhifadhi wa mnyama Faru nchini ameahidi kuendelea kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuwezesha teknolojia za kidijitali na mafunzo kwa askari wanyamapori ili kuendeleza juhudi za muda mrefu za uhifadhi ambazo matunda yake yanaonekana kutokana na ongezeko la Faru nchini kila mwaka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments