WANAFUNZI WATANO WALIOPANDA MSHIKAKI WAFARIKI KWA KUGONGWA NA FUSO CHALINZE


Mfano wa kupanda pikipiki watu wengi 'mshikaki'

Wanafunzi watano wa Shule ya Sekondari Kimange iliyopo Chalinze Mkoa wa Pwani wamefariki dunia baada ya pikipiki waliokuwa wamepanda kwa mtindo wa ‘mshikaki’ kugongwa na gari aina ya fuso.

Akizungumza katika mazishi ya wanafunzi watano waliofariki katika ajali ya gari iliyotokea Agosti 6, 2021 katika eneo la Kimange Chalinze Mkoani Pwani, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani Pwani, Abubakar Kunenge amesema kuwa wanafunzi wanne walifariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na Fuso.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa amesema kuwa, ajali hiyo imetokea Agosti 6, 2021 majira ya saa 1 jioni ambapo gari aina Mitusubishi Fuso yenye namba za usajili T 198 CWN ikitokea Dar es salaam kwenda Arusha lilimgonga mwendesha Pikipiki na kusababisha vifo vya wanafunzi wanne papo hapo na mmoja kufariki akipatiwa matibabu Hospital ya Jeshi Kihangaiko.

Kamanda Nyigesa amesema wanafunzi hao watano wa Kimange Sekondari walikuwa wamepakiana kwenye Pikipiki moja 'Mshikaki' wakitokea Kimange kuelekea Mbwewe na kusema wanafunzi hao walikuwa wakitokea michezoni shule jirani ya Kwamakocho Sekondari.

Kamanda Nyigesa amewataja wanafunzi waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni Laya Masudi (16) mwanafunzi wa Kimange Sekondari Kidato cha tatu, Furaha Athumani (16) Mwanafunzi Kimange Sekondari Kidato cha tatu, Athumani Bushiri (15) Mwanafunzi Kimange Sekondari Kidato cha Kwanza, Amina Msomba (15) Mwanafunzi Kimange Sekondari Kidato cha Kwanza na Athumani Mchafu (17) Mwanafunzi Kidato cha tatu.

KamandaNyigesa ameeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari ambaye alikuwa mwendokasi uliosababisha kushindwa kumudu gari hilo na kupelekea kumgonga mwendesha Pikipiki akiyekuwa mbele yake.


Nyigesa amesema mpaka sasa tayari Jeshi lake limefanikiwa kumshikilia dereva wa gari hilo kwa ajili ya hatua za kisheria.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments