ULEGA ATAKA MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI KUKOMESHWA NCHINI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Handeni, Mkoani Tanga (hawapo pichani) mara baada ya kufika katika wilaya hiypo kwa ziara ya kikazi ya siku moja, Mkoani Tanga. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Handeni, Mkoani Tanga na kutoa maagizo ya kukomeshwa kwa migogoro baina ya wakulima na wafugaji kote nchini, mara baada ya kufika katika wilaya hiyo kwa ziara ya kikazi ya siku moja.  (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).


Na. Edward Kondela

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amewataka viongozi wa maeneo mbalimbali nchini kuanzia ngazi ya kijiji kuhakikisha wanasimamia haki na amani na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kudhibiti migogoro ya wakulima na wafugaji.

 

Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo (12.08.2021) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga na kuibainisha hayoa kwenye kikao chake na uongozi wa wilaya hiyo na kuwataka pia wataalam wa sekta ya mifugo washirikiane vyema na viongozi katika kutoa pia elimu juu ya umuhimu wa makundi hayo mawili ya wakulima na wafugaji.

 

Mhe. Ulega amesema wafugaji lazima waishi kwa upendo maeneo walipo pamoja na wafugaji wengine na wakulima kwa kuwa ni dhambi kubwa kuchukua mifugo na kuingiza kwa makusudi kwenye shamba la mkulima.

 

“Kitendo cha ng’ombe kupelekwa kwenye mashamba ni jinai kama jinai nyingine siyo haki kwa mkulima au mfugaji kuchukua hatua kinyume na taratibu na viongozi wa kijiji wawe wasimamizi wa haki na amani na wasifanye upendeleo pamoja na kufanya vitendo vyovyote vya rushwa.” amesema Mhe. Ulega

 

Naibu Waziri Ulega amelazimika kutoa maelekezo hayo baada ya kupokea taarifa ya uongozi wa Wilaya ya Handeni kuwa kumejitokeza migogoro baina ya wakulima na wafugaji hadi kusababisha vifo vya baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo hali ambayo imekuwa ikisababisha hofu ya mahusiano baina ya makundi hayo mawili.

 

Katika taarifa hiyo wameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inaweka mikakati mbalimbali ya kukomesha migogoro hiyo ambayo imekuwa ikisababisha hofu, ukizingatia Wilaya ya Handeni ina mifugo mingi na imekuwa ikifanya biashara ya kupeleka mifugo ndani na nje ya nchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments