TANZANIA KUNUFAIKA NA UTIAJI SAINI ITIFAKI YA USAJILI NA ULINZI WA HIARI YA HAKI MILIKI


Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godrey Nyaisa akiwa kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Nchi Wanachama wa Shirika la Kanda ya Afrika la Miliki Ubunifu ARIPO, unaofanyika Kampala, Uganda

Washiriki wa Mkutano Mkuu wa wanachama wa Shirika la kanda ya Afrika la Miliki Bunifu, wakiwa katika picha ya pamoja, mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo mapema leo jijini Kampala , Uganda

**********************************

Nchi wanachama wa Shirika la Kanda ya Afrika la Miliki Ubunifu (ARIPO) wamekutana Kampala, Uganda kujadili masuala ya Miliki bunifu Kanda ya Afrika.

Mkutano huo mkuu wa siku tisa uliofunguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Uganda, Mheshimiwa Kiryowa Kiwanuka unafanyika katika hoteli ya Munyonyo jijini Kampala.

Mgeni rasmi amesisitiza ushiriki wa nchi wanachama kujadili kwa kina itifaki hii ili iongeze tija na ufanisi kwa nchi wanachama kwenye kulinda wasanii na kazi zao.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw. Godfrey Nyaisa ambaye anashiriki katika mkutano huo amesema washiriki watajadili na kupitisha Itifaki ya Usajili na Ulinzi wa Hiari wa Haki Miliki kama itaridhiwa na Mawaziri wa nchi wanachama.

"Kwa nchi ya Tanzania, utiaji saini wa Itifaki hii itasaidia wasanii kusajili na kupata ulinzi wa kazi zao nje ya nchi wanachama ambapo ni tofauti na ilivyo sasa msanii akisajili ARIPO anaweza kuomba ulinzi nchi mbalimbali", ameeleza Bw. Nyaisa.

Bw. Nyaisa ameongeza kwa kusema kuwa Itifaki hiyo ya Usajili na Ulinzi wa Hiari ya Miliki Bunifu itasainiwa na Mawaziri wa nchi wanachama wa ARIPO tarehe 27 na 28 Agosti 2021 baada ya kuijadili kwa kina.

BRELA ni taasisi inayosimamia masuala ya Miliki Ubunifu ambayo ni nyanja inayohusu uwezo wa ubunifu wa mtu au watu katika kuunda vitu au kutoa huduma.

Inahusisha masuala ya hataza, tunzi, fasihi na kazi za sanaa, alama kwenye bidhaa na huduma, maumbo ya mikebe ya bidhaa na nyinginezo.

Pia inahusu uwezo wa ubunifu wa binadamu unaotambuliwa chini ya mfumo wa Sheria wa Ulinzi wa Bunifu mbalimbali.

Mbali ya ushiriki wa BRELA washiriki wengine kutoka Tanzania ni Wizara ya Viwanda na Biashara na Chama cha HakiMiliki Tanzania (COSOTA).

Imeandaliwa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano-BRELA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments