SERIKALI YAANZA KUTAFUTA MATOKEO CHANYA YA ZAO LA MWANI

 Na. Edward Kondela
Serikali imesema itaendelea kuwawezesha wakulima wa zao la mwani kwa vifaa pamoja na utaalamu ili waweze kuzalisha kwa wingi na ubora unaohitajika sokoni.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema hayo (01.08.2021) akiwa katika Kijiji cha Zingibari kilichopo Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga, wakati akitoa vifaa vyenye thamani ya Shilingi Milioni Nne kwa ajili ya kilimo cha mwani kwa vikundi vitatu vya wakulima wa zao hilo na kufafanua kuwa serikali itaendelea kutoa bure vifaa hivyo kwa wakulima wa mwani katika mwambao wa pwani ya Bahari ya Hindi ili kuhakikisha zao hilo linalimwa kwa wingi nchini.

Akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Tanga, Mhe. Ndaki amesema kutokana na zao la mwani kuwa la kiuchumi kwa wananchi wa mwambao wa pwani ya Bahari ya Hindi, serikali imeanza kuweka mazingira mazuri ya uwezeshaji na kutafuta masoko ya uhakika ili wakulima waweze kunufaika kiuchumi.

"Huu msaada wa vifaa kwa ajili ya kilimo utafika katika maeneo yote yenye uzalishaji na msisitizo tumeanza kuweka kwenye elimu ya namna ya kulima zao la mwani kwa ajili ya tija zaidi." amesema Waziri Ndaki

Aidha, Waziri Ndaki akiwa katika Kata ya Kipumbwi Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga, amesema serikali inatarajia kutumia Shilingi Bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa soko la kimataifa katika kata hiyo kwa ajili ya kuuza dagaa ndani na nje ya nchi.

Mhe. Ndaki amesema wanunuzi wa dagaa wanaotoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Malawi, Rwanda na Burundi wataenda kununua dagaa kutoka Kipumbwi hivyo wafanyabiashara wa kata hiyo hawatapata shida ya kutafuta soko la dagaa.

“Niwaambie serikali imesikia na inakusudia kujenga kujenga soko la kimataifa la kuuza dagaa, msipate shida kuuza dagaa wenu.” Amesema Waziri Ndaki.

Amesema kwa kipindi kirefu wakazi wa Kata ya Kipumbwi wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa masoko ya dagaa wanaopatikana katika eneo hilo na kwamba wamekuwa wakivua dagaa kwa wingi.

Kuhusu uvuvi haramu Waziri Ndaki amesema serikali itavunja Vikundi vya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) ambavyo vitabainika kujihusisha na uvuvi haramu na kuhakikisha viongozi wa vikundi hivyo wanafikishwa Katika vyombo vya sheria.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema imebainika baadhi ya viongozi wa BMU wanajihusisha na wavuvi kushiriki vitendo vya uvuvi haramu katika maziwa pamoja na Bahari ya Hindi.

“Baadhi ya BMU zimeshindwa kutekeleza wajibu wake na kushirikiana na wavuvi haramu acheni mara moja kabla hamjakumbana na mkono wa sheria, yeyote atakayematwa anajihusisha na uvuvi haramu atachukuliwa hatua kali za kisheria.” Amesema Mhe. Ndaki

Katika ziara hiyo ya kikazi ya siku moja Mkoani Tanga, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amekagua pia majengo ya Vikundi vya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika Wilaya za Mkinga na Pangani, yaliyojengwa kupitia mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH).

Katika sekta ya mifugo, Waziri Ndaki pia ametembelea mnada wa mpakani wa Horohoro kujionea miundombinu mbalimbali inayowekwa kabla ya kuanza rasmi kwa mnada huo ambao anasema utakuwa na matokeo chanya pindi utakapokamilika.

“Licha ya kusaidia kupunguza utoroshaji wa mifugo mnada utasaidia kuongeza kipato kwa wananchi na hivyo kuinua uchumi wao, kwa sababu wakipeleka ng’ombe nje ya nchi wanauza bei ya juu lakini pia tunataka tuwapunguzie wananchi adha ya kuvuka mipaka kwani jambo hili wakati mwingine linasababisha kuuza mifugo yao kwa bei ya chini.” Amesema

Hata hivyo Waziri Ndaki amesema wameamua kuondoa shida hizo kwa kuwa na minada ya mipakani ili wafugaji waweze kuuza mifugo yao maeneo rasmi na serikali iweze kupata mapato yao.

Akizungumza katika nyakati tofauti kwenye ziara hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema wizara ina malengo ya kuhakikisha wananchi wanaohusika na sekta ya uvuvi wananufaika kupitia rasilimali zinazopatikana katika Bahari ya Hindi pamoja na maziwa yaliyopo nchini huku kwa kuwa serikali itaendelea kuwasaidia kwa kila hali likiwemo suala la vifaa pamoja na marekibisho ya sheria na tozo mbalimbali.

Nao baadhi ya wananchi wamesema wamefurahishwa na ziara ya kikazi ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki kwa kuwa imeendelea kujibu changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika sekta ya uvuvi pamoja na kuwatafutia fursa zilizopo kupitia sekta hiyo.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post