AVEMARIA BUGULASHI: MJIOLOGIA WA BARRICK MWENYE NDOTO YA KUFIKIA VIWANGO VYA KIMATAIFA


AveMaria Bugulashi
AveMaria Bugulashi (kwanza kushoto) akitoa maelezo kwa Waziri wa Ardhi.Mh.William Lukuvi alipotembelea banda la Barrick katika maonesho ya Sabasaba 2021.

 ***
-Atoa wito kwa vijana wa kitanzania kutoogopa masomo ya sayansi

“Kutokana na kuzaliwa katika mkoa wenye shughuli za uchimbaji wa madini nilijikuta tangu nikiwa mdogo nilitamani nikikua nifanye kazi zinazohusiana na madini, nilipokuwa shule ya sekondari ndoto yangu ilikuwa kusoma masomo yanayohusiana na fani hiyo, nashukuru ndoto yangu imetimia”, anasema Avemaria Bugulashi.

Avemaria Bugulashi, ni mtaalamu wa sekta ya madini katika mgodi wa kampuni ya Barrick wa North Mara, mwenye cheo cha Productive & Reconciliation Geologist, ambaye anaamini kuwa bado sekta ya madini inayo fursa kubwa ya kukuza uchumi wa Tanzania na kuwataka vijana wa kitanzania kutoogopa kusomea fani za sayansi ikiwemo utafiti wa madini ili ziwe na wataalamu wa kutosha.

Katika mahojiano hivi karibuni alisema kuwa alihitimu shahada yake ya kwanza ya Geology mwaka 2007 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo mwaka uliofuata aliajiriwa na kampuni ya Barrick kama Graduate Geologist na baada ya hapo amekuwa akipanda daraja hadi kufikia nafasi aliyonayo hivi sasa.

“Najivunia kufanya kazi kazi na kampuni kubwa ya madini kama Barrick ambapo nimeweza kujifunza mambo mengi kuhusiana na masuala ya utafiti wa madini kupitia mafunzo mbalimbali ya ndani na nje ikiwemo kufanya kazi na wataalamu waliobobea katika fani hii”,anasema.

Anasema kuwa Barrick imewekeza kwa kiasi kikubwa katika matumizi ya teknolojia za kisasa na mifumo ya uchimbaji madini inayotumika katika migodi mingine yote mikubwa duniani kiasi kwamba matumizi ya teknolojia yanafanya kazi kuwa rahisi.

Pia anasema kuwa kampuni Imekuwa ikijali wafanyakazi wake kwa kuwapatia maslahi mazuri na kutoa motisha mbalimbali ambazo zinawafanya wajisikie vizuri na kuwa na maendeleo yao binafsi na familia zao.

“Kampuni pia inazingatia viwango vya kimataifa vya afya na usalama katika maeneo yake ya kazi kiasi kwamba tunafanya kazi katika mazingira mazuri na salama japo tupo sehemu za migodi ambazo bila kuzingatia kanuni za usalama zina uwezekano wa kuwa na ajali nyingi”,anasema.

Anatoa wito kwa kampuni kutoa fursa za wanawake wengi migodini tofauti na sasa ambazo kazi nyingi zinafanywa na wanaume na kuwataka wanawake kujiamini na kuchangamkia fursa za ajira zinapotokea mahali popote na kuondoa dhana kuwa kuna baadhi ya kazi zinapaswa kufanywa na wanaume pekee.

Matarajio yake ya baadaye, anasema anatamani kuwa Mjiolojia (Geologist) wa kimataifa hivyo, atazidi kujiendeleza zaidi kielimu Ili ndoto yake hiyo itimie. Anafurahia mafunzo mbalimbali ya ndani ambayo yanazidi kumjengea uwezo wa kumudu kazi yake vizuri na kuaminika.

Kuhusu mambo anayopendelea nje ya kazi yake anasema anapendelea kukaa na familia yake,kufanya mazoezi na kusoma vitabu na majarida mbalimbali mtandaoni yanayohusiana na fani yake. "Kutokana na mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia ni muhimu kusoma mambo mbalimbali ili usibaki nyuma",alisema.

Mtazamo wake kuhusu sekta ya madini nchini Bugulashi, anaamini pia kuwa sekta hii inazidi kukua, makampuni na wananchi wengi wanapenda kujihusisha na uchimbaji wa madini mbalimbali yaliyopo nchini. Aliipongeza Serikali kwa jitihada inazofanya kuhakikisha madini yanayochimbwa yananufaisha wananchi pia wawekezaji katika sekta hii wanatoa ajira kwa watanzania.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments