MBISSO : TUME YA UTUMISHI WA UMMA NI MATOKEO YA MABORESHO YA SERIKALI KUUFANYA UTUMISHI WA UMMA UONGEZE UFANISI NA UWAJIBIKAJI





Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. John Mbisso (kulia) akitoa ufafanuzi wakati wa Kikao cha Kazi cha Tume na Wadau kujadili Mpango Mkakati, Mkoani Morogoro kushoto ni Bw. David Pwele, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji.
Picha ya pamoja ya Washiriki kutoka Tume ya Utumishi wa Umma na Wadau kujadili Mpango Mkakati wa Tume, Kikao kinachofanyika Mkoani Morogoro.
 ***
Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. John Mbisso amesema kuwa Tume ni matokeo ya maboresho mbalimbali yaliyoanzishwa na Serikali kwa lengo la kuufanya Utumishi wa Umma uongeze ufanisi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Bwana Mbisso amesema haya jana Mkoani Morogoro wakati wa Kikao kazi cha Tume na wadau kujadili Mpango Mkakati wa Tume ya Utumishi wa Umma ulioandaliwa wa kipindi cha mwaka 2021/22 hadi 2025/2026.

Amesema kuwa pamoja na malengo makuu ya Sera ya Menejimenti na Ajira ya mwaka 1999, kukabiliana na changamoto mbalimbali katika Utumishi wa Umma, Sera hii ililenga pia kuunganisha Tume tofauti zilizokuwepo na kuunda Tume moja ya Utumishi wa Umma ambayo ingesimamia taratibu zote za ajira na nidhamu katika Utumishi wa Umma.

“Madhumuni ya kuundwa kwa Tume ya Utumishi wa Umma ilikuwa ni kuhakikisha kuwa Utumishi unakuwa mmoja na watumishi wote wana taratibu za usimamizi, hadhi, haki na maslahi yanayofanana” amesema Bwana Mbisso.

“Jukumu la msingi la Tume ni kurekebu (regulate) Utumishi wa Umma nchini ili kuimarisha utawala bora na uwajibikaji kwa Viongozi na watumishi wa ngazi zote katika Utumishi wa Umma. Aidha, Tume inasimamia, kufuatilia na kutathmini uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia Utumishi wa Umma nchini. Kazi kubwa ya Tume ni kufuatilia na kusimamia uendeshaji wa shughuli za Rasilimali Watu katika Taasisi za Umma, kuhakikisha kuwa Utumishi wa Umma unaendeshwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu, pamoja na kupokea na kushughulikia rufaa za watumishi wa umma kupinga maamuzi yaliyotolewa na Mamlaka zao za Nidhamu” alifafanua Bw. Mbisso.

Bw. Mbisso alihitimisha kwa kusema kuwa, Tume itaendelea kutekeleza majukumu yake iliyonayo chini ya Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298 (marejeo ya mwaka 2019) katika kuhakikisha kuwa Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka za Nidhamu katika Utumishi wa Umma zinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayotolewa ili azma ya Serikali ya kuwa na Utumishi wa Umma uliotukuka iweze kufikiwa

Imeandaliwa na:

KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI

TUME YA UTUMISHI WA UMMA

MOROGORO

07 AGOSTI 2021

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments