ASKOFU GWAJIMA, SILAA WASIMAMISHWA KUHUDHURIA VIKAO VYA BUNGE


Mbunge wa Kawe Mhe. Josephat Gwajima

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamebariki maamuzi ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambayo imependekeza azimio la kutaka Mbunge wa Kawe Askofu Josephat Gwajima kutohudhuria mikutano miwili ya bunge mfululizo.

Azimio hilo limetolewa leo Agosti 31, 2021 bungeni na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Emmanuel Mwakasaka ambaye ni mbunge wa Tabora mjini.

''Kamati ilijiridhisha kuwa kauli alizotoa Mbunge wa Kawe Askofu Josephat Gwajima, zinadhalilisha bunge, zinaonesha dharau na kushusha hadhi na heshima ya bunge, shughuli za bunge na uongozi, hivyo tunaliomba bunge kumsimamisha kutohudhuria mikutano miwili mfululizo pamoja na kumpeleka azimio kwa chama chake ili kimchukulie hatua'' - Emmanuel Mwakasaka, Mkiti kamati ya Maadili.

Aidha Mwenyekiti huyo wa Kamati aliongeza kuwa, ''Moja ya jambo ambalo kamati ililiona ni utovu wa nidhamu uliokithiri kwa mbunge Josephat Gwajima na kosa kama hilo kwa mujibu wa kanuni za bunge ni mbunge asihudhurie mikutano mfululizo isiyopungua miwili au isiyozidi mitatu''.
Mbunge wa Ukonga Jerry Silaa

Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge pia imetoa azimio kuhusu shauri la mbunge wa Ukonga Jerry Silaa asimamishwe kuhudhuria mikutano miwili mfululizo ya bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akisoma azimio hilo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Emmanuel Mwakasaka ambaye ni mbunge wa Tabora mjini amesema mbali na kusimamishwa pia aondolewe kwenye uwakilishi wa bunge la Tanzania katika bunge la Afrika.

''Kamati ilimhoji Mh. Jerry Silaa ili kuthibitisha kauli yake kuwa mishahara ya wabunge haikatwi kodi na aliuzwa iwapo mshahara wake unakatwa kodi au haukatwi alisema kuna sehemu inakatwa kodi na kuna sehemu haikatwi kodi'' - Emmanuel Mwakasaka, Mwenyekiti kamati ya Maadili.

Mwakasaka ameongeza kuwa, ''Katika mahojiano Mh. Jerry Silaa alikiri kuwa kauli zake zimeleta tafrani kwenye jamii, uchambuzi wa ushahidi wa sheria kwenye shauri hili unathibitisha kuwa alikuwa na nia ovu ya kulidharau na kulidhalilisha bunge pamoja kuchonganisha bunge, serikali, uongozi wa bunge na wananchi''.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post