RC MTAKA AZINDUA CHANJO YA CORONA DODOMA....ATAKA WANAOPOTOSHA WAPUUZWE

Mkuu  wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka akichanjwa chanjo ya Corona

Na Dotto Kwilasa, Dodoma.

SIKU chache baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuzindua Kitaifa  chanjo ya ugonjwa wa Uviko -19 Jijini Dar es Salaam, Mkuu  wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amezindua chanjo hiyo kimkoa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo huku akiwatoa wasiwasi wananchi kuwa chanjo hiyo haina madhara kwao.

Hayo yanajiri  huku kukiwa na maneno mengi ya upotoshaji yakiendelea kwenye mitandao ya kijamii kuwa chanjo hiyo ni ya majaribio na kwamba ina madhara kwa afya ya binadamu  na kusababisha hofu kwa baadhi ya wanachi kuhusu zoezi hilo la Chanjo.

Akiongea wakati wa uzinduzi huo Jijini Dodoma Mtaka amesema,"Kuna upotoshaji mwingi sana ambapo wengine wanasema viongozi wanachanja maji huu ni uongo na upotoshaji,wapo ambao wanasema hawachanji lakini wanasubiri wakahonge hela hospital ili wapatiwe cheti nawaambia mtakuja kunikumbuka,"

Katika kudhihirisha umuhimu wa chanjo hiyo,Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma ameeleza kuwa tangu  mwaka huu uanze ameshapoteza ndugu zake  20 kwa ugonjwa wa Corona na kwamba hadi sasa bado kuna wengine familia inaendelea kuwauguza.

"Naongea kwa uchungu nawaomba ndugu zangu mkubali kuchanjwa kujizuia na Ugonjwa huu,ni kweli upo na unaua na mimi ni mhanga kwa kuwa nimeondokewa na watu wangu wa karibu 20, hivyo kwa sasa tunahamasishana kuchanja lakini badae tutaanza kuchanja kwa kimemo", amesema Mtaka.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Jabir Shekimweri ametumia nafasi hiyo  kumpongeza Rais Samia kwa kuweza kuitikia kiu ya watanzania nakuongeza kuwa mitandao ya kijamii inatoa taarifa nyingi sana hivyo watu wanatakiwa kuchagua taarifa na kuifanyia kazi.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Best Magoma amesema kuwa kama mkoa wamepokea chanjo elfu 50 ,lakini pia anashukuru kuwepo kwa mwitikio wa wananchi .

"Tuna jumla ya vituo 28 ambavyo vimetengwa kwaajili ya kutoa chanjo mkoani Dodoma,ambapo vituo  7 vipo katika halmashauri ya jiji la Dodoma na halmashauri nyingine 6 zimepelekewa dawa katika vituo vitatu vitatu",alisema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments