WAZIRI KABUDI AWATAKA WATUMISHI WA WIZARA YAKE KUSHIRIKI KATIKA MAJUKUMU NA KUTATHMINI UTEKELEZAJI WAKE


Na mwandishi maalum, Morogoro.
Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi amewataka watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria kushiriki katika utekelezaji wa majukumu ya wizara na kutathmini mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu hayo kwa pamoja ii kuleta tija na ufanisi ndani  ya Wizara.

Prof.Kabudi alikuwa akizungumza na watumishi hao alipokuwa akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo lililofanyika mkoani Morogoro.

“Ni vyema kila mtumishi akashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa pamoja kama timu na kutathmini mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu ya Wizara,” alisema.

Prof. Kabudi pia amewataka watumishi hao kuhakikisha wanasoma na kuielewa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 -2025 na kupanga kuitekeleza, kufahamu vipaumbele vya serikali ya Awamu ya Sita na jinsi vinavyopaswa kutekelezwa, kujitambua, kutambua nafasi  na majukumu yao ndani ya Wizara na kuwa na  utendaji kazi wa pamoja kama timu.

Prof Kabudi pia ametaka kila mtumishi  wa Wizara  kushiriki katika utendaji kazi wa pamoja na kushiriki katika ujengaji wa taswira ya Wizara ili kuwa na taswira inayoendana na mabadiliko ya nchi inavyokwenda ikiwa ni pamoja na kuongeza kasi ya kutangaza shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wizara ili umma upate kufahamu.

Amewataka watumishi hao kuhakikisha wanazingatia na kufuata sheria, taratibu na kanuni za Serikali kuwa waadilifu katika mawasiliano na kuongeza na kuimarisha mawasiliano na mashauriano ya kazi ndani ya Wizara ili kumfanya kila mtumishi kuelewa mambo yanayotekelezwa.

Prof. Kabudi pia amewapongeza watumishi hao kwa kutembelea ili kujionea kwa pamoja utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya ujenzi wa Bwawa la kufua Umeme wa Mwalimu Julius Nyerere huko Rufiji mkoani Pwani na Ujenzi wa Reli ya Kisasa kutokea  mkoani Morogoro – Kilosa hadi Dodoma na kuwasihi wawe mabalozi wazuri kuelezea yanayoendelea katika miradi hiyo na kuendelea kuiunga mkono Serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria walitembelea miradi ya ujenzi wa Bwawa la kufua Umeme wa Mwalimu Julius Nyerere huko Rufiji mkoani Pwani na walipokuwa njiani kurejea jijini Dodoma walitembelea Ujenzi wa Reli ya Kisasa unaoendelea kutokea Morogoro – Kilosa hadi Dodoma


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments