MKAKATI WA KOPA MBUZI LIPA MBUZI KUANZA, CHANJO ZA MIFUGO ZATAKIWA VIJIJINI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), (kushoto) akipewa maelezo na mmoja wa wanasanyansi wanaotengeneza chanjo ya Tatu Moja Prof. Phillemon Wambura namna chanjo hiyo inayodhibiti magonjwa ya mdondo, ndui na mafua ya kuku isivyoweza kughushiwa kwa namna yoyote ile kwa kuwa imewekewa rangi maalum ya kubaini endapo ikiwa imeghushiwa. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akionesha namna chanjo ya Tatu Moja inayozalishwa na kampuni ya Nobel Vaccine Bioscience (NOVABI) inavyotumika kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mdondo, ndui na mafua ya kuku kupitia njia ya kwenye macho ya mifugo hiyo. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akitoa maelekezo kwa uongozi wa Ranchi ya Mkata iliyopo Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro, kuhakikisha wanazalisha mbuzi wengi zaidi kwa ajili ya mkakati wa kopa mbuzi lipa mbuzi ili wananchi wengi zaidi waweze kuingia katika ufugaji wa kisasa na kibiashara. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiwa ameshika moja ya aina ya mbuzi wanaozalishwa kwenye Ranchi ya Mkata iliyopo Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogororo mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya siku moja katika ranchi hiyo na kuagiza ranchi hiyo kuendeleza uzalishaji wa mbuzi kwa ajili ya kufuga kibiashara. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Na. Edward KondelaSerikali imesema Ranchi ya mifugo ya Mkata iliyopo Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro itakuwa sehemu ya kuzalisha mbuzi kwa wingi kwa ajili ya mkakati wa kopa mbuzi lipa mbuzi ambao unatarajia kuanza hivi karibuni lengo likiwa ni kuwa na mbuzi wa kutosha kwa ajili ya soko la nje ya nchi.

Akizungumza na uongozi wa ranchi na Wilaya ya Kilosa, wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja katika Ranchi ya Mkata, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalllah Ulega amesema ni muhimu kuangalia namna bora ya kufanya ufugaji wa kibiashara katika ranchi hiyo.


Amesema serikali imechagua Ranchi ya Mkata kuwa kituo cha kuzalisha mbuzi kwa wingi ambacho watakuwa wanasambaza katika maeneo mbalimbali nchini.


"Tutakayempa tutataka tujue yupo wapi na ana mbuzi wangapi ili tuwatambue na tuwaingize katika mfumo wetu wa takwimu za kibiashara ili iwapo tunapata mteja wa kilo 50 kwa mwezi kweli tuwe na uhakika wa kupata kilo hizo 50 kwa mwezi.” Amesema Mhe. Ulega

Kutokana na mkakati huo wa kopa mbuzi lipa mbuzi mahitaji ya mbuzi yatakuja kuwa makubwa nchini hivyo ameitaka ranchi hiyo kuzalisha mbuzi kwa wingi ili kuweza kutosheleza soko la ndani na nje ya nchi.

Aidha Mhe. Ulega amesema wafugaji wa mbuzi wafuge kibiashara ili kuweza kutimiza vigezo na masharti ya wateja wa kimataifa kama nchini hizo na kutolea mfano wa nchi za uarabuni ambazo wanataka mbuzi wenye uzito wa kilo kati ya 8 hadi 10 ambao hawajakomaa sana.

Kwa upande wake Meneja wa Ranchi ya Mkata Bw. Oscar Magete amesema ranchi ilianzishwa na serikali kwa madhumuni ya kuendeleza na kueneza ufugaji bora wa mbuzi, kondoo na ng'ombe ambapo ranchi hiyo kwa sasa ina mbuzi 609 kondoo 116 na ng'ombe 47.


Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ulega ametembelea kiwanda cha kuzalisha chanjo cha Nobel Vaccine Bioscience (NOVABI) kilichopo Mkoani Morogoro kinachozalisha chanjo aina ya Tatu Moja kwa ajili ya ya mdondo, ndui ya kuku na mafua ambayo yanaathiri mfumo wa upumuaji na yamekuwa chanzo kikuu cha vifo vya kuku na kuwatia hasara wafugaji.


Akiwa kiwandani hapo Naibu Waziri Ulega ameelekeza chanjo hiyo ya kipekee isambazwe maeneo mbalimbali nchini hususan vijijini ambapo kuna wafugaji wengi wa kuku wa kienyeji ili waweze kuipa mifugo yao chanjo kuondokana na hasara ambayo wamekuwa wakipata ya kuku kufa kutokana na magonjwa hayo.

Ameongeza kuwa ni vyema uongozi wa wizara kuhakikisha chanjo mbalimbali zinazozalishwa ndani na nje ya nchi zinawafikia walengwa hususan waliopo vijijini ili waweze kufuga kibiashara na waweze kunufaika kupitia mifugo yao.

 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post