DC KISWAGA AMALIZA SAKATA LA MGAMBO NA MACHINGA KAHAMA.... "VIJANA MSISHINDANE NA SERIKALI"


Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Festo Kiswaga

Na Malunde 1 blog - Kahama
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Festo Kiswaga ameelekeza kuachiwa huru kwa Wafanyabiashara wawili wa Matunda Rasta na Jofley walioshikiliwa kwa kosa la kushambulia askari wa Manispaa ya Kahama waliokuwa wakitimiza wajibu wao.

Mhe. Kiswaga ametoa msamaha huo mapema leo Jumapili Julai 18,2021 alipotembelea na kuongea na wajasiriamali wa Soko la Matunda na Machinga lililopo eneo la CDT Mjini Kahama.

"Nimetoa msamaha kwenu ili iwe funzo kwenu na kuwapa nafasi ya kujirekebisha, serikali ina malengo makubwa kwa vijana.. Serikali inataka muwe pamoja, muunde vikundi vingi ili kama hamna mitaji iwakopeshe, na mikopo inayotolewa na Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan haina ubaguzi wa itikadi za vyama, uwe Chadema, iwe CUF, NCCR au CCM wote ni wa Tanzania, ni marufuku kwa machinga kufirisika.. " amesema Kiswaga.

Mhe. Kiswaga amesema ziara yake kwenye eneo hilo imetokana na kuona kipande cha Video kilichokuwa kinasambaa mitandaoni kikionesha Mgambo wa Manispaa ya Kahama wakibeba bidhaa za muuza matunda aliyekuwa akifanya biashara pembezoni mwa barabara.

"Unajua mitandao ya Kijamii ina nguvu sana, na jambo linasambaa kwa haraka sana kupitia mitandao hiyo, nlipoona hiyo video hiyo nikawasiliana na viongozi lakini sijaridhishwa na maelezo yao na ndiyo maana nimekuja hapa, ila kwa maelezo ya Mheshimiwa Diwani na viongozi wa Machinga nimejiridhisha kuwa wale vijana walikuwa na makosa, ila tunawapa nafasi nyingine..na nakuagiza kiongozi wa eneo hili kuwapatia hawa eneo la kufanyia biashara zao ndani ya eneo hili ambalo lipo rasmi kwa kazi hiyo..na Mkurugenzi ameweka wazi kuwa ikifika saa moja jioni mnaruhusiwa kwenda huko barabarani lakini asubuhi na mchana eneo la biashara ni hili.." amesema Kiswaga.

Amewataka wafanyabiashara wadogo wadogo hususani wauza matunda kufuata sheria walizozitunga na kutokuwa na tabia ya kushindana na serikali kwa maamuzi ambayo yanaweza kuwahatarishia uchumi wao.

Katika hatilua nyingine Mhe. Kiswaga amewaasa askari wa Manispaa ya Kahama kufanya jukumu lao la msingi la kulinda wafanyabiashara wafanye biashara kwa amani badala ya kuwabughudhi na kuwapa hofu na inapotokea changamoto kabla hawajachukua hatua wawasiliane na viongozi kwanza.

Kwa upande wao wafanyabiashara hao waliokumbwa na hiyo kadhia wamemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa Msamaha na wameahidi kutii na kufuata sheria zilizowekwa na Serikali.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama Underson Msumba amesema serikali ipo kwajili ya wananchi kwa kuboresha miundombinu rafiki na kuwataka wakulima kwenda kuchukua pesa za mikopo ili kukuza uchumi wao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments