WAKULIMA MILIONI MBILI WASAJILIWA KUPITIA MFUMO WA M-KILIMO


Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema wizara imefanikiwa kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu utambuzi wa wakulima ambapo hadi sasa kupitia Mfumo wa M-Kilimo tayari wakulima 1,979,662 na Maafisa Ugani 6,840 wamesajiliwa kwenye mfumo hatua inayosaidia kufikisha huduma za ugani na masoko kwa haraka.


Bashe ametoa kauli hiyo jana(04.07.2021) wakati alipoongea na Waandishi wa habari ofisini kwake Dodoma ambapo amesema lengo la wizara ya kilimo ni kusajili wakulima takribani milioni 6 kupitia kaya zao hatua itakayosaidia utambuzi na ufikwishwaji wa huduma za ugani ili kuwezesha tija kwenye kilimo kupatikana.


Aliongeza kusema kuwa ili wizara iweze kuwahudumia wakulima ni lazima kuwatambua na kufahamu mahala walipo ndio maana ikaanzisha mfumo wa kiteknolojia wa usajili wa wakulima (M-Kilimo) ambao sasa umefika mikoa yote ya Tanzania Bara.


" Katika bajeti ya mwaka 2021/22 wizara imepanga kufundisha maafisa ugani (re-training) ili waweze kusaidia wakulima kuongeza tija kwenye uzalishaji mazao ambapo ili lengo hilo lifanikiwe lazima uwatambue wakulima ndio maana tumeanzisha mfumo huu wa Mobile Kilimo ambapo wakulima wanasajiliwa kupitia maafisa ugani kwenye kata." aliema Bashe.
Akizunguza juu ya umuhimu wa mfumo huo Naibu Waziri Bashe alisema mfumo M-Kilimo utasaidia kupima kazi zaMaafisa ugani Kilimo katika maeneo ya kiutendaji kwa kuwa takwimu zinaonesha kila ushauri alioutoa kwa mkulima ikiwa ni wa ana kwa ana (physical consultation) au kupitia njia ya mtandao (online consultation).


“ Hadi sasa jumla ya maswali ya wakulima yapatayo 7,792 yamepokelewa na kujibiwa na maafisa Ugani Kilimo kupitia mfumo wa M-Kilimo unaoratibiwa na Wizara ya Kilimo” alisisitiza Bashe na kuongeza kuwa wizara inatarajia kufungua kituo cha huduma kwa wakulima (Call Centre) kuwezesha wakulima kupiga simu na kujibiwa maswali yao kwa haraka zaidi.


Katika hatua nyingine Bashe ametaja mikoa iliyofanya vizuri kwenye usajili wa wakulima kuwa ni Morogoro (153,977), Njombe (153,158) na Mara (148,772) huku mikoa ambayo bado ipo chini ikiwa ni Pwani imesajili wakulima 14,784) na Mtwara (28,000) .


Kufuatia hatua hiyo Bashe ametoa wito kwa wakurugenzi wa halmashauri nchini kuwawezesha maafisa ugani wao wa wilaya kusajili na kuhamasisha wakulima ili waingie kwenye mfumo wa M-Kilimo kuwezesha kufikia lengo la kukuza tija kwenye uzalishaji mazao ya kilimo kupitia huduma bora za ugani.


Ili kuleta ufanisi kwenye usajili wa wakulima Naibu Waziri huyo wa wizara ya Kilimo alisema kupitia bajeti 2021/22 inatarajia kununua simu za mkononi za kisasa (smartphones ) na kuzigawa kwa Maafisa Ugani kote nchini ili zitumike kusajili wakulima  kwa kutumia teknolojia maalum (App)


Naye Mratibu wa Mfumo wa M-Kilimo Rajab Mkalange amesema mfumo huu ni wa kiteknolojia unaoweza kumsaidia mkulima kupata huduma za ugani na masoko kupitia maswali kwenye simu yake ya kiganjani kuwasiliana na Afisa Ugani ngazi za kijiji, kata, wilaya na Wizarani.


Aliongeza kusema mfumo huu tangu uliopanza kufanya kazi mwanzoni mwa mwaka huu umewezesha kupunguza tatizo la upungufu wa maafisa ugani kwa kuwa wakulima wanaweza kupata huduma hizo pale wanapokuwa wamesajiliwa kwenye mfumo.


Kwa upande wake Mkuu wa Mifumo ESRF John Kajiba alisema taasisi yake ilifanya utafiti kwenye mikoa ya Kagera na Mara kuhusu mahitaji ya wakulima kwenye huduma za ugani na kugundua kuwa wakulima wanahitaji taarifa za huduma za ugani na masoko kwa haraka kutaboresha tija kwenye Kilimo.


Kajiba aliongeza kusema kuwa kupitia utafiti huo ndipo wakaanzisha ushirikiano na Wizara ya Kilimo kuanzisha mfumo wa M-Kilimo unaotekelezwa kote nchini .


Wakulima wanaweza kujiunga na Mfumo wa M-Kilimo kupitia simu zao za mkononi ambapo wanaweza kubonyeza *152*00# na kuchagua neon Huduma za Serikali kisha kubofya namba 7 Kilimo.


Mwisho
Imeandaliwa na :
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments