Breaking

Post Top Ad

Saturday, July 3, 2021

YANGA YAIDUNGUA SIMBA SC 1-0 RAIS SAMIA AKISHUHUDIA KILA KITU
Derby imemalizika, Yanga wanafanikiwa kuzuia ubingwa wa mapema kwa Simba.

Kikosi cha Yanga, leo kimeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Didier Gomes.

Mchezo wa leo ambapo Simba SC ilikuwa inahitaji pointi tatu ili kutangazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara mambo yalikuwa magumu kwa timu hiyo iliyoshuhudia pointi tatu zikienda Yanga.

Ni Zawadi Mauya ambaye alikuwa shujaa wa mchezo kwa kupachika bao moja mbele ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu na kuwafanya Simba wasiamini wanachokiona.

Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha jumla ya pointi 70 ikiwa nafasi ya pili huku Simba ikibakiwa na pointi 73 baada ya kucheza jumla ya mechi 30.
Rais was Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa katika Uwanja wa Mkapa kushuhudia mchezo wa Simba dhidi ya Yanga.

Rais Samia amewasili majira ya Saa 10:57 jioni ikiwa ni dakika moja kabla timu hazijaingia Uwanjani kwa mchezo.

Hii inakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais Samia kuhudhuria mechi ya Ligi Kuu Bara tangu awe Rais wa Awamu ya sita.

Mara baada ya kuwasili Rais Samia alikwenda moja kwa moja juu kuketi huku maelfu ya mashabiki wa timu zote wakimshangilia kwa kelele sambamba na kumpigia makofi.

Rais Samia amepokelewa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallece Karia akiwa amekaa naye pamoja katika eneo la wageni maalum.

Kuwasili kwa Rais Samia kulifuta ratiba ya awali ambayo ilikuwa inamfanya Waziri wa Maji Juma Aweso kuwa mgeni rasmi kama ilivyotangazwa mapema na timu mwenyeji wa mchezo wa leo Simba.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages