WATUMISHI TISA WA AFYA WASIMAMISHWA KAZI UWANJA WA NDEGE DAR KWA KUTOKUFIKA KAZINI KUTOA HUDUMA YA VIPIMO VYA CORONA


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Watumishi tisa wamesimamishwa kazi katika Kitengo cha upimaji wa COVID - 19 kwa wasafiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere (JNIA).

Agizo hilo limetolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Abel Makubi alipofanya ziara uwanjani hapo kukagua utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa juzi alipofika hapo akiwa ameambatana na Katibu mwenzake wa Wizara ya Uchukuzi.

Prof. Makubi amesema hakufurahishwa na kitendo cha utovu wa nidhamu, kilichofanywa na watumishi cha kutokufika kazini bila kutoa taarifa rasmi kwa uongozi hapo jana na leo.

"Jana watumishi wanane hawakufika na leo mmoja bila kutoa sababu ya msingi, jumla wanakuwa tisa," amebainisha.

Ameongeza "Imeonekana hapa hili zoezi la baadhi ya watumishi kutokuja kazini limekuwepo, sasa hii imenisikitisha sana kwa baadhi ya viongozi kushindwa kuchukua hatua zinazostahili na kulindana kwa kuficha uozo.

"Kwa hiyo hawa ambao hawakufika jana ambao jumla walikuwa wanane na kati yao wanne walikuwa wameajiriwa na Wizara ya Afya na wanne wameajiriwa na Manispaa ya Dar es Salaam, wapo chini ya RAS wa Dar es Salaam.

"Nimeagiza hawa walio chini ya Wizara ya Afya wasimame kufanya kazi ili tufanye uchunguzi na kuchukua hatua stahiki.

"Huu ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu ambapo mtumishi anaamua kuacha kuja kazini na kusababisha usumbufu kwa wenzake na abiria ambao wanakuja hapa kwa sababu yeye 'gap yake haijawa covered' na mtu yeyote," amesisitiza.

Prof. Makubi ameongeza "Lakini vile vile ambao wameajiriwa na Ofisi ya RAS nitashauri mamlaka husika nao wachukuliwe hatua hivyo hivyo ambazo zimechukuliwa kwa hawa wa Wizara.

Amesema Serikali haiwezi kuvumilia watumishi wasio na nidhamu na wanaodharau majukumu wanayopewa.

"Hizo ndizo hatua ambazo tumechukua, lakini pia tutahakikisha tutaleta wengine 'ku-replace' hao tisa waweze kuendelea ili tusije tukaathiri hizi shughuli za upimaji hapa 'airport'," amesema.

Ametoa onyo kwa watumishi wa afya nchini, wawe tayari kufanya kazi popote pale watakapopangiwa.

"Waende wakafanye kazi siyo kwamba ukipelekwa upande mmoja unaamua kususia kama hawa ambavyo waliamua ni kwa sababu walihamishwa kutoka kwenye vituo vyao vya awali wameletwa huku.

Amewataka watumishi wote wa afya kutanguliza uzalendo wa hali ya juu katika utendaji wa kazi zao na kwa kujituma.

"Hapa tunapofanya upimaji, ni upimaji unawakilisha sura ya Nchi yetu. Kwa hiyo mtu yeyote anayeletwa hapa maana yake ndiye anayetoa taswira ya nchi yetu kwa ujumla.

"Anavyohudumia wasafiri, customer care yake na yeye mwenyewe kujibidiisha wanapofika hapa. Niwaombe watumishi ni vizuri watangulize uzalendo katika kazi zao lakini pia kuwajibika kwa kile walichopangiwa kwa kujitoa ili kuepusha malalamiko kwa wananchi.

"Najua watumishi wengi wanaojituma ila kwa hawa wachache niwaombe wazingatie uzalendo, uwajibika na 'customer care' nzuri wanapohudumia wananchi," ameagiza.

Awali, Prof. Makubi amesema maelekezo waliyoyatoa na Katibu mwenzake wa Wizara ya Uchukuzi yametekelezwa ikiwamo la kuongeza watumishi katika eneo la upimaji.

"Nimefarijika kuna maboresho zaidi yamefanyika, hasa hasa kuongeza sehemu za kupima lakini pia maeneo ambayo abiria wanaweza kuwa wanapimwa.

"Nimeona wameongeza upande mmoja ambao abiria watakuwa wanaingia wakifuata mstari na pia kwa umbali wa mita moja moja kwa kuachana.

"Lakini pia upande wa kushoto na kwenyewe nimekuta kumeongezwa maeneo ambayo watakuwa wanaingia na kupimwa na kuna watumishi 20 tumeongeza kama tulivyokuwa tumeongea siku zile," amesema.

Amesema watumishi hao wameongezeka kulingana na ongezeko la abiria.

"Kwa sababu mwanzoni abiria walikuwa wachache sasa hivi wamekuwa wengi, kwa hiyo kama Wizara tumeweza kuhakikisha kwamba ile changamoto waliyokuwa nayo ya watumishi ili waweze kuendana na abiria imeweza kutekelezwa, wameshafika na wamefanyiwa 'orientation' ili waweze kufanya kazi na wenzao" amesema.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Abel Makubi akizungumza baada ya kutembelea uwanja wa ndege wa kimataifa wa JNIA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments