RASILIMALI WATU NI RASILIMALI MUHIMU KULIKO RASILIMALI NYINGINE



Baadhi ya Maafisa wa Tume ya Utumishi wa Umma wakimsikiliza Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Nyakimura Muhoji (hayupo pichani) leo wakati wa Kuhitimisha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2021, Kikao kilichofanyika Jijini Dar es Salaam. (Picha na PSC).
Baadhi ya Maafisa wa Tume ya Utumishi wa Umma wakimsikiliza kwa makini Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Nyakimura Muhoji (hayupo pichani) leo alipozungumza na Watumishi wa Tume wakati wa kuhitimisha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Jijini Dar es Salaam. 
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Lington N. Ngaikwela (aliyesimama) akizungumza na watumishi wa Tume leo wakati wa kuhitimisha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Kikao kilichofanyika Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Bw. Nyakimura Muhoji, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma. (Picha na PSC).

*************************

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Nyakimura Muhoji amesema nchi yetu ikiwa na Rasilimali Watu iliyosimamiwa na kujiendesha vizuri hata rasilimali nyingine za Taifa zitasimamiwa vizuri kwa kuwa Rasilimali Watu ndiyo husimamia rasilimali nyingine zote.

Bwana Muhoji amesema haya leo Jijini Dar es Salaam katika Kikao na Watumishi wa Tume kuhitimisha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2021. Amesema kuwa Tume ya utumishi wa Umma ni sehemu muhimu katika kufikia malengo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo ya mwaka 2025 katika Uimarishaji wa Utawala Bora kwenye eneo la Usimamizi wa Masuala ya Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma.

“Kazi zenu mnazofanya zinahusu masuala ya rasilimali watu, maisha ya watu na zinahitaji uadilifu mkubwa, zikifanyika vizuri, tutaweza kutoa mchango wetu kwa kiwango kikubwa kwa kuimarisha Uwajibikaji na Utawala Bora katika Utumishi wa Umma. Nchi yetu ikiwa na Rasilimali Watu iliyosimamiwa na kujiendesha vizuri hata rasilimali nyingine za Taifa zitasimamiwa vizuri kwa kuwa Rasilimali Watu ndiyo husimamia rasilimali nyingine zote” ,amesema Bwana Muhoji.

Kwa upande mwingine amesema, kupitia maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma tunayohitimisha leo ni muhimu sana kukumbushana umuhimu wa kutekeleza wajibu wetu kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zinazotawala katika Utumishi wa Umma.

“Nitoe wito kwenu, endeleeni kuchapa kazi kwa bidii katika kutekeleza majukumu yenu kwa kuzingatia Sheria zilizopo, fanyeni kazi zenu kwa maarifa, weledi, uadilifu, umakini na moyo wa kujituma, eleweni kuwa kazi zenu mlizoaminiwa mkakabidhiwa mkizitekeleza vyema zitawajengeeni heshima kubwa” amesema Bw. Muhoji. 

Bwana Muhoji alisema kuwa, mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alielekeza Viongozi katika Taasisi za Umma kutenda haki kwa watumishi walio chini yao na watumishi wote wa umma kutoa huduma bora kwa Wananchi.

“Watumishi wa Tume mnapaswa kuhakikisha wakati wote mnatekeleza kazi zenu kwa kuzingatia maadili ya utumishi wenu na mara kwa mara jielekezeni katika kupata matokeo chanya katika utekelezaji wa majukumu yenu katika sehemu zenu za kazi, changamoto zipo hazikosekani zigeuzeni changamoto kuwa fursa” alisema Bw. Muhoji.

Alihitimisha kwa kutoa rai kwa watumishi wa Tume kuwa wakati wanatekeleza majukumu yao watekeleze kwa kiwango cha juu wawe na umoja na mshikamano uwe ni endelevu.

“Kikubwa kwenu ni kuchapa kazi kwa maarifa yenu yote, kuweni wabunifu, zungumzeni pale panapohitaji majadiliano, tumieni utaalam wenu kushauri, tambueni kuwa mmeaminiwa kuwa Tume na kupewa dhamana ya kufanya kazi za Tume, kila mmoja wenu katika nafasi yake naamini waliowapa waliwaamini. Kumbumbeni siku zote usemi unaosema “Ukiaminiwa, Aminika” alisisitiza Bw. Muhoji.

Katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza tarehe 16 hadi 23 Juni 2021. Tume ilikutana na watumishi wa umma na wadau waliopo katika Wilaya ya Kisarawe Mkoani Pwani na Dar es Salaam na maeneo mengine, ambapo watumishi wa Tume walitoa huduma ya kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi changamoto za kiutendaji za kiutumishi kutoka kwa Watumishi wa Umma na Wadau.

Miongoni mwa masuala yaliyotolewa ufafanuzi katika maadhimisho haya ni kuhusu Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298 (marejeo ya mwaka 2019), rufaa na malalamiko, likizo, upandishwaji vyeo, mafunzo pamoja na namna ya kushughulikia masuala ya nidhamu kwa watumishi wa umma wanaotuhumiwa kufanya makosa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments