NAIBU WAZIRI KIPANGA: SERIKALI IMEWEKA NGUVU KATIKA KUBORESHA VYUO VYA UALIMU

 Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe.Omari Juma Kipanga amesema serikali ipo kwenye mikakati ili kuhakikisha wanafunzi wanaopata ujauzito wanarudi kuendelea na masomo yao baada ya kujifungua.

Ameyasema hayo leo katika kongamano la wadau na wachangiaji wa elimu lililofanyika katika Chuo Kikuu Cha Dar es salaam (UDSM) likiwa na lengo kujadili na kuweka mikakati ya pamoja itakayowezesha kuzitatua changamoto zinazoikabili Sekta ya elimu nchini.

Aidha Mhe.Kipanga amesema suala la kupata elimu ni haki kila mtanzania hivyo utaratibu utawekwa ili kuhakikisha waliopata ujauzito wanarejea kuendelea na masomo.

“Pamoja na jitihada za kukarabati na kujenga miundombinu mbalimbali lakini pia serikali imeweka nguvu katika kuboresha vyuo vya ualimu ili viweze kuzalisha walimu watakoendana na kasi ya Teknolojia”, amesema Kipanga.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi. Bahati Geuzye amesema zaidi ya shilingi Bilioni 9.1 zilitumika kufadhili miradi 96 ya elimu katika shule 88 na taasisi moja ya sayansi na teknolojia kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya shule 116 zinanufaika na miradi  123 inayogharamia jumla ya shilingi Bilioni 9.4.

Bi. Geuzye amesema kuwa jukumu la msingi la mfuko wa Elimu wa Taifa unaoratibiwa na TEA ni kuongeza jitihada za serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu nchini kwa lengo la kuongeza ubora wa elimu na upatikanaji wake wa usawa.

“Kupitia mfumo huu taasisi za elimu kuanzia ngazi ya shule za msingi, shule za Sekondari, vyuo  vya kati na vyuo vya Elimu ya juu vinapata fursa ya kufadhiliwa miradi inayolenga kuboresha mazingira na kujifunza na kujifunzia”,amesema Bi.Geuzye.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments