Tanzia : RAIS WA KWANZA WA ZAMBIA KENNETH KAUNDA AFARIKI DUNIA...HII HAPA HISTORIA YAKE | MALUNDE 1 BLOG

Thursday, June 17, 2021

Tanzia : RAIS WA KWANZA WA ZAMBIA KENNETH KAUNDA AFARIKI DUNIA...HII HAPA HISTORIA YAKE

  Malunde       Thursday, June 17, 2021

Mmoja ya watu maarufu zaidi barani Afrika na mpiganiaji uhuru, Kenneth Kaunda ameaga dunia nchini Zambia akiwa na umri wa miaka 97.

Kaunda maarufu kama KK alikuwa rais wa kwanza wa Zambia huru.

Alikimbizwa katika hospitai moja mjini Lusaka mapema wiki hii na kulazwa baada ya kuugua homa ya mapafu.

Mwaka 1950 , bwana Kaunda alikuwa mtu muhimu katika Vuguvu la kupigania uhuru wa Rhodesia ya kaskazini kutoka kwa Uingereza.

'Nahuzunika kusema kwamba tumempoteza Mzee', mwana wa Kaunda Kambarage , aliandika katika ukurasa wa facebook wa babaake akiwataka wafuasi wake kumuombea babake.

Rais wa Zambia Edgar Lungu amesema kwamba taifa hilo lilikuwa likimuomboleza mtoto mwa wa Afrika.

''Niligundua kwamba umefariki leo mchana nikiwa na majonzi makubwa'', aliandika katika facebook.

'Kwa niaba ya taifa lote na kwa niaba yangu naomba kwamba familia yote ya Kaunda inafarijika wakati tunapomuomboleza rais wetu wa kwanza na mwana wa Afrika'''.

Kalusha Bwalya, nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Zambia amesema kwamba Kaunda amefanya mengi nchini humo. "

Alikuwa Rais wa kwanza wa Zambia mwaka 1964 na kuongoza taifa hilo kupitia miongo kadhaa ya utawala wa chama kimoja.

Alijiuzulu baada ya kupoteza katika uchaguzi wa vyama vingi 1991.

Bwana Kaunda alikuwa shabiki mkubwa wa juhudi za kumaliza ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

Alikuwa pia akiongoza mavuguvugu nchini Msumbiji na nchini Zimbabwe.

Kenneth David Kaunda (anafahamika zaidi kama KK).

Siku chache zilizopita, Dk. Kaunda alilazwa katika Hospitali ya Maina Soko jijini Lusaka kufuatia maradhi yaliyokuwa yanamsumbua kwa siku kadhaa.

Kaunda aliyezaliwa April 28, 1924, aliitawala Zambia kuanzia mwaka 1964 hadi mwaka 1991
Kenneth Kaunda alikuwa ni mmoja wa viongozi waasisi wa Afrika mpya, wakati nchi yake ilipoondokana na ukoloni na kuwa taifa huru.

Kiongozi huyu ambaye alikuwa na haiba ya uchangamfu, alisifiwa kama kiongozi aliyekuwa na msukumo wa kisasa katika bara licha ya kwamba mwanzoni aliikataa dhana ya demokrasia ya vyama vingi.

Akiwa mwana wa Afrika aliyejitolea, alianza kazi ya kuijenga Zambia mpya, huru kuamua njia yake katika masuala ya kimataifa.

Lakini usimamizi duni wa uchumi ulisambabisha umaarufu wake kushuka, na akaondolewa madarakani baada ya kushindwa kwa kura wakati uchaguzi huru ulipofanyika mwaka 1991.


Kenneth David Kaunda alizaliwa tarehe 28 Aprili 1924 katika kituo cha wamishonari karibu na mpaka baina ya Rhodesia Kaskazini (Zambia ya sasa) na Congo.
Kaunda alishawishiwa sana sera za Martin Luther King (kushoto)

Baba yake, ambaye alikuwa mchungaji aliyetawazwa na kanisa la Uskochi- Church of Scotland alifariki alipokuwa bado mtoto, na kuiacha familia katika hali ya dhiki.

Lakini uwezo wa Kaunda mdogo wa kielimu ulimpatia fursa katika shule ya kwanza ya sekondari iliyoanzishwa kaskazini mwa Rhodesia, na baadaye akawa mwalimu.

Kazi hiyo aliifanya katika jimbo la Copperbelt na Rhodesia Kusini, ambayo kwa sasa ni Zimbabwe, ambako kwa mara ya kwanza alipata uzoefu, na kuchukizwa sana na athari za utawala wa wazungu.

Moja ya vitendo yake ya kisiasa ilikuwa ni kuto kula nyama kama njia ya kupinga sera ambayo iliwalazimisha Waafrika kwenda kwenye dirisha lililotengwa kwa ajili yao kwenye vichinjio vya kununua nyama.

Mwaka 1953 alikuwa katibu mkuu wa vuguvugu la Northern Rhodesian African National Congress lakini vuguvugu hilo lilishindwa kuwahamasisha Waafrika dhidi ya shirikisho tawala la wazungu la Federation of Rhodesia na Nyasaland.

Kaunda akiwa katika kipindi cha BBC Brains Trust mwaka 1960

Miaka miwili baadaye alifungwa, na adhabu kali, kwa kusambaza vijikaratasi ambavyo mamlaka ilioviona kama upinzani.

Kwa kukata tamaa na kile alichokiona kama kushindwa kwa chama chake kuchukua msimamo mkali wa haki za wazawa Waafrika, Kaunda alianzisha chama chake cha Zambian African National Congress.

Katika kipindi cha mwaka mmoja, kilipigwa marufuku na Kaunda alirejeshwa tena gerezani. Kufungwa kwake kulimfanya ageuke kuwa mkali.

Kufikia mwaka 1960 alikuwa amekuwa kiongozi wa chama kipya cha United National Independence Party (Unip) na kwa kuchochewa na shauku iliyofuatia ziara ya kumtembelea Martin Luther King nchini Marekani, alianza mpango wake wa uasi wa raia ambao ulihusisha kufungwa kwa barabara na kuchoma majengo.

Kaunda alisimama kama mgombea wa Unip katika uchaguzi wa mwaka 1962 ambapo muungano ambao haukuwa raihisi uliundwa na African National Congress (ANC) uliochukua mamlaka katika bunge.
Alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Rhodesia Kaskazini mpya iliyoundwa

Shirikisho la Rhodesia na Nyasaland lilivunjwa mwishoni mwa mwaka 1963 na mwezi mmoja baadaye, Kaunda alichaguliwa kama waziri mkuu wa Northern Rhodesia. Nchi ilioewa jina upya kama Zamia, ikapata uhuru kamili Oktoba 1964 na Kaunda kama rais wake wa kwanza.

Kaunda alianza kwa faida ya kuongoza taifa la Afrika lenyemsingi imara wa uchumi kuliko nchi nyingine yoyote jirani lakini kulikuwa na upungufu wa Wazambia wazawa waliokuwa na ujuzi na mafunzo ya kuendesha nchi.

Msimamo wake pia uliathiriwa pakubwa na azimio la pamoja la uhuru katika Rhodesia Kusini.

Upinzani wa kisiasa

Sera ya vikwazo iliyowekwa na serikali ya Uingereza dhidi ya nchi iliyojitenga ilionekana walau kama kuudhuru uchumi wa Zambia.

Katika hali hiyo, Kaunda alibaini kuwa inaendelea kuwa vigumu kuendeleza sifa yake ya kwa kiasi - ingawa miito yake ya kulitaka jeshi la Uingereza ya sauti ya juu kuliko wale viongozi wa mataifa mengine ya ambao maslahi yao hayakutishiwa moja kwa moja.

Mnamo mwaka 1969, kwa gharama kubwa, alitaifisha migodi ya shaba, ambayo iliipatia nchi 90% ya mapato ya fedha za kigeni. Lakini bei ya shaba ilianguka, bei za mauzo ya ya petroli inayoagizwa nje iliongezeka, na uchumi, tayari uliokuwa umedhoofika , ulikuwa karibu kuwa tatizo kubwa.
Kuanguka kwa bei ya shaba kulidhoofisha uchumi wa Zambia

Wakati wa uhuru Zambia ilikuwa mojawapo ya nchi tajiri zaidi duniani katika mataifa yaliyopo kusini mwa jangwa la Sahara, lakini kufikia mwaka 1991 ilikuwa na deni la dola bilioni 8.

Kaunda hakuchelewa kuchukua msimamo mkali dhidi ya upinzani wa kisiasa. Mnamo mwaka 1972 alitangaza taifa la chama kimoja, hali ambayo haikutulia mpaka mwaka 1991, wakati uchaguzi huru ulifanyika.

"Ingekuwa ni balaa kwa Zambia kama tungeingia mfumo wa vyama vingi," aliwahi kusema wakati mmoja, "kwasababu vyama hivi vingetumiwa na wale wanaopinga ushiriki wa Zambia katika mapambano ya uhuru."

Mageuzi ya amani

Kama mwenyekiti wa mataifa sita yaliyo mstari wa mbele katika kampeni dhidi ya ubaguzi wa rangi, aliongoza upinzani kwanza kwa Ian Smith katika Rhodesia na baadaye dhidi ya utawala nchini Afrika Kusini.

Hahahivyo, aliendelea kufanya kazi katika makazi katika Rhodesia, na alikuwa na mikutano na viongozi wa Afrika Kusini John Vorster, PW Botha na FW de Klerk.

Aliwahifadhi wakimbizi wa kisiasa kutoka Afrika Kusini na katika nchi yakena alipambana na Margaret Thatcher, hususan juu ya kupinga kwake vikwazo dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi. Lilikuwa ni suala ambalo lilitishia hali ya baadaye ya Jumuiya ya madola.

Alishirikiana na viongozi wa Afrika Kusini kupata suluhu ya tatizo la Rhodesia

Katika wigo mpya wa siasa za Afrika alikuwa mwanasiasa wa kadri, aliyejitolea kwa jamii nyingi , na kila mara alikuwa na matumaini ya mageuzi ya amani ambayo yatawapatia nafasi waafrika wazungu pamoja na weusi.

Kinyume na wengine, alibakia kuwa mtetezi mkuu wa sera rais wa Zimbabwe Robert Mugabe ya mageuzi ya ardhi, mbayo chini yake wakulima wazungu walifurushwa nje ya nchi, iliyosababisha kuporomoka kwa uchumi wa nchi.

"Nimekuwa nikisema wakati wote, tafadhali msimlaumu Robert Mugabe. Sisemi mbinu anazozitumia ni sahihi, lakini alikuwa amewekewa shinikizo kubwa."

Alikataliwa

Nyufa zilianza kuonekana katika utawala wa Kaunda mwishoni mwa mwaka 1980. Kulikuwa na ripoti za majaribio ya kupindua serikali yake, na amri ya kutotoka nje usiku iliwekwa katika maeneo mengi ya nchi.

Katika kipindi cha miaka 10 iliyofuatia, majaribio mengine mawili ya kumpindua yaliripotiwa. Jjaribio la mwisho, lilikuwa la mwaka 1990, kufuatia ghasia katika katika mji mkuu , Lusaka, na jimbo la Copperbelt , dhidi ya mpango wa serikali wa kunusuru uchumi.

Zaidi ya watu 20 waliuawa katika ghasia za siku tatu, na vikosi vya usalama vilivamia Chuo kikuu cha Zambia na kukifunga kuzuia ghasia.

Wakati alipokwenda Cuba mwaka 1989 nguvu zake za mamlaka zilikuwa zimepungua

Kaunda alikuwa anakabiliwa shinikizo linaloongezeka kutoka ndani ya Zambia na kutoka kote duniani kuanzisha demokrasia ya kweli. Hatimaye alikubali na akaitisha uchaguzi tarehe 31 Oktoba 1991.

Kuanzia wakati kampeni ilipoanza, ilikuwa wazi kwamba alikuwa mashakani, na kulikuwa mshangao kidogo wakati wapiga kura walipomkataa na kuchagua vuguvugu la demokrasia ya vyama vingi, lililoongozwa na Frederick Chiluba.

Lakini alikuwa bado ana ushawishi mkubwa katika Zambia na serikali mpya ilimuona kama tisho.

Kaunda alikamatwa na kushitakiwa kwa mashitaka ya uhaini mwaka 1997 ingawa serikali mpya ililazimika kuondoa mashitaka hayo baada ya shinikizo la kimataifa.

Jaribio la baadaye la kumtangaza kama mtu asiye na uraia hatimaye lilitupiliwa mbali na mahakama.
Alikuwa mshirika wa karibu wa hayati kiongozi wa Zimbabwe Robert Mugabe

Aligeuza mwelekeo wake katika mapambano dhidi ya HIV na Ukimwi na alikuwa kiongozi wa kwanza wa Kiafrika kukiri kuwa mmoja wa watoto wake wa kiume, Masuzyo, alikufa kutokana na Ukimwi.

Akiwa mwandishi mahiri, alichapisha vitabu kadhaa vilivyoelezea fikra za ujamaa wa Afrika, ambayo ilifuatwa na viongozi wengine wa Afrika ikiwa ni pamoja na Kwame Nkrumah nchini Ghana na Julius Nyerere nchini Tanzania.

Mbali na siasa Kaunda alikuwa mchezaji densi mashuhuri, na katika mwaka 2011, alionekana kama mmoja wa hadhira yenye shauku katika onyesho la Dancing with the Stars, toleo la kimataifa la tamasha la Strictly Come Dancing.
Kaunda alikuwa mmoja wa viongozi wapya wa Afrika walioondosha ukoloni.

Pia alikuwa mcheza gitaa na alitunga nyimbo za ukombozi ambazo alizicheza alipokuwa akisafiri nchini mwake kutafuta uungaji mkono kwa ajili ya kampeni dhidi ya utawala wa kikoloni.

Kenneth Kaunda aliepuka kwa kiasi kikubwa ugomvi ambao ulionekana katika mataifa mapya mengine yaliyopata uhuru na kufanikiwa katika kuunganisha sehemu za nchi yake chini ya kauli mbiu -One Zambia, One Nation.

Lakini sera yake ya uchumi iliigeuza nchi ambayo ilikuwa na uwezekano wa kuwa na mapato makubwa kuwa taifa ambamo umasikini uliendelea kusambaa na muda wa matarajio ya maisha ulikua miongoni mwa viwango vya chini zaidi duniani.

CHANZO - BBC SWAHILI

Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post