RPC MUSILIMU : WALIOPANGA KUFANYA UHALIFU MOROGORO HAWATATOKA SALAMA


Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro SACP Fortunatus Musilimu

Na Jackline Lolah Minja - Morogoro

Jeshi la polisi Mkoa wa Morogoro limetoa onyo kwa wahalifu ambao wamepanga kuingia kwenye mkoa huo kuacha mara moja na endapo watafanikiwa kuingia hawatatoka salama.

Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro SACP Fortunatus Musilimu ametoa onyo hilo leo Mei 11 2021 wakati akitoa taarifa juu ya msako na doria zinazofanywa na jeshi hilo ambapo amesema hawatasita kuchukua hatua kwa wahusika wa vitendo vya uhalifu akibainisha kuwa wamefanikiwa kukamata watuhumiwa 108 wa makosa mbalimbali.

"Nitoe onyo kwa wahalifu wote ambao wanafikiria au wamepanga kuja kufanya uhalifu Mkoani Morogoro kuacha mara moja, endapo watafanikiwa kuingia Morogoro wajue hawatatoka salama. Wahalifu hawa wengine wanakuja na silaha wakati wananchi hawana silaha. Silaha ni jeshi la polisi hivyo kwanza tutazichukua hizo silaha,sisi wenyewe ndiyo tunajua jinsi ya kuchukua silaha hizo", amesema Kamanda Musilimu.

"Natoa taarifa misako na oparesheni hii ya safisha safisha uhalifu Morogoro, itaendelea katika maeneo mbalimbali yakiwemo nyumba za wageni na  baa zote za Morogoro , na Operesheni hii inashirikisha jamii, vikundi vya ulinzi shirikishi , kampuni za ulinzi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama",amesema

Amesema Jeshi la polisi mkoani humo limekamata makosa hatarishi ya barabarani 481 ikiwemo madereva 42 kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani na  hatua za kisheria zimechukuliwa na  madereva wa nne wamefungiwa leseni zao.

"Doria na oparesheni zitaendelea kufanyika barabarani kwa watakaoendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa au ku-overtake pamoja na madereva wasiofuata alama na michoro ya barabarani, pamoja na waendesha pikipiki wasiovaa kofia na watakaopakia abiria wawili (mishikaki ) nao tutawakamata na hatua kali zitachukuliwa dhidi yao",ameeleza.

 Hata hivyo kamanda Musilimu amesema anawashukuru wadau wote wanaoshirikiana na jeshi la polisi katika kutoa taarifa za uhakika juu ya wahalifu na amewaomba kuongeza ushirikiano zaidi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments