Utaratibu Mbovu Kuigharimu Benki Iwapo Fedha Za Mteja Zitaibwa


 Na. Peter Haule na Saidina Msangi, WFM, Dodoma
Serikali imesema kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hutoa adhabu kwa Benki yeyote itakayobainika kusababisha fedha za mteja kuibwa kutokana na utaratibu uliowekwa na Benki husika kuwa na kasoro.

Hayo yamebainishwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi, Hamad Yussuf Masauni (Mb), alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Jang’ombe, Bw. Ali Hassan King, aliyehoji wizi unapotokea kwenye akaunti ya benki ya mteja uliofanywa na mtumishi wa benki nani mwenye wajibu wa kumlipa mteja.

“Endapo itabainika kuwa wizi umefanywa na mtumishi wa Benki, hatua stahiki huchukuliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo ikiwa ni pamoja na mteja kulipwa kiasi alichoibiwa”, alisema Mhandisi Masauni.

Alieleza kuwa mhalifu huchukuliwa hatua za kinidhamu pamoja na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ili Sheria ichukue mkondo wake.

Mhandisi Masauni alibainisha kuwa, wizi unapotokea kwenye akaunti ya benki ya mteja, uchunguzi wa kina hufanywa na vyombo husika katika masuala ya upelelezi ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kadri hali na mazingira ya tukio yatakavyokuwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments