MWENYEKITI WA HALMASHAURI TARIME AZUIA SARUJI 1,800 ZILIZOGANDA KWA FEDHA ZA CSR


Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Simion Samweli akikagua tofari zinazodaiwa kutokuwa na ubora

Na Dinna Maningo, Tarime
MWENYEKITI wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Simion Samwel ambaye pia ni Diwani kata ya Nyakonga amezuia saruji zaidi ya 1,800 zilizonunuliwa kwa fedha ya uwajibikaji wa makampuni kwa jamii (CSR) zinazotolewa na mgodi wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya uchimbaji wa dhahabu ya Barrick baada ya kuganda kutokana na kukaa mwaka mzima bila kutumika.

Samwel aliyasema hayo wakati wa ukaguzi wa baadhi ya miradi inayotekelezwa kwa fedha za CSR akiwa ameongozana na Mwenyekiti wa kamati ya uchumi na ujenzi ambaye ni Diwani wa kata ya Matongo Godfrey Kegoye, Mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii  Steven Gibai ambaye ni Diwani wa kata ya Manga na Kaimu Muhandisi ujenzi halmashauri ya wilaya ya Tarime  ambaye pia ni fundi sanifu ujenzi John Phabian.

Aliongeza kuwa mbali na saruji hizo zilizoganda amebaini uwepo wa matumizi mabaya ya fedha baada ya kukuta vifaa vingi vikiwa vimezidi mahitaji yaliyokusudiwa zikiwemo saruji huku miradi hiyo ikishindwa kukamilika kwa wakati,gharama kubwa za manunuzi na matumizi makubwa ya fedha kwenye miradi ikilinganishwa na uhalisia.

Samwel alisema kuwa amezuia saruji hizo kutotumika kwakuwa zimekwisha ubora na endapo zikitumika majengo hayatakuwa imara hali ambayo inaweza kuisababishia hasara halmashauri kutoa fedha zingine kukarabati majengo. 

"Mimi na Wenyeviti wa kamati tuliamua kuzunguka kutembela ujenzi wa miradi ya elimu na afya kwa fedha za CSR tulipofika kijiji cha Nyakunguru tulikuta saruji mifuko 334 ikiwa imeganda na vifaa vingine vikiwa vimehifadhiwa kwa muda mrefu zaidi ya mwaka bila kutumika, vingine vimebaki,hii ni hasara na matumizi mabaya ya fedha haiwezekani saruji zimeganda alafu ziendelee kutumika huu ni uzembe wa halmashauri ambao ndiyo wasimamizi wa miradi inayojengwa kwa fedha za CSR.

"Kama mwenyekiti wa halmashauri na wenyeviti wa kamati tumezuia isitumike kwanza tukalijadili hili kwenye vikao vyetu ikiwezekana halmashauri ipeleke saruji zingine pesa watajua watakakozitoa wenyewe maana ni uzembe wa mkurugenzi na wataalamu wake kwasababu sisi tumeingia halamshauri mwaka huu na miradi hii ni ya mwaka 2018 na hadi sasa haijakamilika",alisema Samwel.

Diwani wa kata ya Kibasuka Thomas Nyagoro alisema kuwa zahanati ya Itandura ilijengwa kwa nguvu za wananchi majengo yake yamechakaa kwakuwa ina zaidi ya miaka 30 haitumiki bila kutoa huduma yoyote na haijasajiliwa.

Akisoma taarifa kwa Mtendaji wa kijiji cha Nyakunguru Zakayo Wangwe alisema kuwa Mgodi wa North Mara ulitoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya mganga, ukarabati wa zahanati, ujenzi wa kichomea taka na placenta piti, ujenzi wa choo na barabara. 

"Ujenzi wa nyumba 1 pacha ya mtumishi utakao gharimu fedha milioni 88,734,528.17,ukarabati wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) sh. milioni 32,662,872.00,ujenzi wa choo cha nje matundu 21 sh.Milioni 19,289.617.30,ujenzi wa kichomea taka na placenta piti sh. Milioni 11,091,750.00 na sh. Milioni tatu  kama gharama za usimamizi kwa kamati ya ujenzi na wataalamu, jumla ya fedha zote za mradi wa zahanati ni sh Milioni 154,778,767.47",alisema.

Mwenyekiti wa kijiji cha Nyakunguru Chacha Makuri alisema kuwa fedha hizo ni za mwaka 2018,hawajapokea fedha za CSR kwa mwaka 2019 -2020 nakwamba walipokea mradi mwingine wa barabara kutoka barabara ya Nyakato -Turuturu km 7,barabara ya Nyakunguru senta -Nyamuma wa sh Milioni 55 lakini mradi huo ujenzi umekuwa ni wakusuasua.

"Hii miradi fedha zinatolewa na mgodi na wasimamizi ni halmashauri wao ndiyo wanaandaa BOQ na kufanya manunuzi sisi ni kupokea vifaa na kuwasimamia mafundi,mafundi wana suasua halmashauri inatuletea fundi ambaye anakuwa na tenda nyingi anashindwa kumaliza kwa wakati ukimuuliza anakwambia hujamwajili yeye mwajili wake ni mkurugenzi ndiye anatakiwa amuhoji,hizi saruji tulizipokea julai, 2020 hadi sasa hazijatumika zimeganda",alisema Makuri.

Mwenyekiti wa kitongoji Cha Itandura Masero Matiko alisema kuwa Mgodi una nia nzuri ya kusaidia jamii lakini usimamizi wa miradi ndiyo unakwamisha ujenzi kutokamilika kwa wakati huku Chacha Chacha yeye akisema tatizo siyo Fundi tatizo ni pesa kutolipwa kwa wakati hali inayosababisha vibarua kukimbia ambapo yeye kama kibarua wa kuchanganya udongo anamdai fundi sh 50,000/= tangu Novemba 2020.

Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi kijiji cha Nyakunguru aliwalalamikia wataalamu wa ujenzi kutoka halmashauri kutofika kwa wakati kukagua ujenzi na kusababisha miradi kujengwa chini ya kiwango,kuwapa kazi mafundi wasio na uwezo wa kifedha kuchukua mafundi wa bei ya chini wasioweza kukamilisha kazi kwa wakati. 

"Halmashauri imetenga fedha za usimamizi kwa kamati ya ujenzi na wataalamu milioni tatu lakini hawafiki kuna huyu fundi sanifu ujenzi anaitwa Isaya huyu ni tatizo ukimpigia simu kuwa kuna sehemu fundi kajenga vibaya au tofari siyo nzuri anakuambia piga picha nitumie kwa whatsapp sasa mimi simu yangu ni ndogo kasimu katochi nitaitumaje huku kijijini wengi tunatumia simu za tochi, mmeshuhudia tofari zinavyopukutika tofari linalouzwa kwa sh 1,500 wao wanasema wamenunua kwa sh 2,500,ukiona jengo la milioni 88 utashangaa wizi mtupu",alisema. 

Bhoke Marwa mkazi wa Nyakunguru alisema kuwa zahanati hiyo ikifanya kazi itawasaidia kwani wanalazimika kutembea umbali km 7 kuifuata huduma ya afya kituo cha afya Nyarwana hali inayosababisha wajawazito kujifungulia njiani na wagonjwa wengine kufia njia wakati wakitembea kwenda kufuata huduma ya afya. 

Mwenyekiti huyo wa halmashuri na wenyevikiti wa kamati walitembelea ujenzi wa shule mpya ya sekondari Matongo nakukuta ujenzi wa madarasa matatu ukiendelea utakaogharimu zaidi ya Milioni 88 huku mifuko ya saruji 570 iliyoganda ikiwa imetunzwa. 

Kaimu Mwenyekiti wa kijiji Cha Matongo Charles Ryoba alisema kuwa mfumo unaotumika katika pesa za CSR ni mbaya nakwamba badala ya halmashauri kuhusika kwenye michakato ya manunuzi serikali za vijiji ndiyo vihusike katika michakato ya manunuzi ,usimamizi na halmashauri hivisimamie vijiji kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na siyo kila kitu kushughulikiwa na halmashauri. 

 Wakiwa katika shule ya msingi Murito walikuta zaidi ya saruji 200 na vifaa vingine vikiwa vimetunzwa ndani ya darasa wanalosomea wanafunzi wa darasa la nne huku katika hospitali ya halmashauri ya wilaya kukiwa kumehifadhiwa saruji mifuko 650 ikiwa imeganda.

Diwani wa kata ya Kemambo Rashid Bogomba alisema kuna madarasa mawili shule ya Murito yanajengwa yatakayo gharimu Milioni 63 nakwamba changamoto ni mbao kupinda baada ya kukaa muda mrefu bila bati kuezekwa na saruji kuganda. 

Mwenyekiti wa kamati ya uchumi na ujenzi Godfrey Kegoye alisema kuwa kuna miradi ya CSR iliyojengwa tangu 2017 lakini hadi sasa haijakamilika licha yakutakiwa kukamilika ndani ya miezi sita,ujenzi kuwa chini ya kiwango,vifaa kununuliwa kwa gharama kubwa Nakwamba yeye kama mwenyekiti wa kamati hajaridhishwa na ujenzi wa miradi ya fedha za CSR licha ya miradi hiyo kugharimu fedha nyingi. 

Mwenyekiti wa kamati ya huduma ya jamii Steven Gibai alisema kuwa usimamizi wa miradi siyo mzuri nakwamba watahakikisha wanasimamia vyema miradi hiyo na itakayokuwa chini ya kiwango hawatokubari kukaa kimya wataisemea ili kuhakikisha inakuwa na ubora.

Kaimu Muhandisi wa halmashauri ya wilaya hiyo John Fabian alisema kuwa idara ya ujenzi haina gari na wakati mwingine analazimika kutumia gharama zake kwa usafiri wa pikipiki au kutumia usafiri wa gari la mgodi wanapokuwa wakiitembelea miradi ya fedha wanazozitoa za CSR. 

 Alisema kuwa saruji ikikaa kwa zaidi ya miezi 6 bila kuhifadhiwa sehemu salama upungua ubora na kuharibika,akashauri saruji hiyo isitumike kwenye ujenzi na upigaji wa ripu badala yake itumike kuweka jamvi sakafuni au kufyatua tofari.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Apoo Tindwa alikiri kuwepo kwa changamoto ya ufujaji wa fedha katika idara ya ujenzi na manunuzi nakwamba ameshachukua hatua kwa kuwaandikia barua baadhi ya watendaji nakwamba wakithibitika kwa ufujaji wa fedha watachukuliwa hatua na kuwa baadhi ya mafundi waliochelewesha kazi wamekamatwa.

Alisema kuwa kitendo cha fundi mmoja kupewa kazi nyingi na kusababisha miradi kuchelewa kukamilika kwa wakati ni uzembe wa idara ya ujenzi wakiwemo wahandisi kutokagua miradi kwa wakati nakusababisha baadhi ya miradi kujengwa chini ya kiwango. 

Hata hivyo baadhi ya mafundi wakuu waliopewa kazi za ujenzi wa miradi ambao hawakutaka kutajwa majina walidai kuwa fedha wanazopewa haziendani na kazi, kwani huambiwa kiasi fulani kutokana na mikataba yao na halmashauri lakini wakifuatilia fedha siyo halisi kwa mujibu wa mikataba.

Walieleza kuwa wakifatilia mgodini fedha zinazotolewa ni zaidi ya kiasi kilichopo kwenye mikataba yao na wakipungukiwa fedha wakiomba kuongezewa hawapewi na wakati mwingine hawalipwi fedha kwa wakati wakifatilia hutishiwa  kutopewa kazi  hali inayosababisha miradi kutokamilika kwa wakati na kujengwa kwa ubora ikilinganishwa na fedha halisi zinazotolewa na mgodi. 
Mifuko ya Saruji ikiwa imehifadhiwa kwenye chumba cha darasa la nne katika shule ya msingi Murito kata ya Kemambo ikiwa imeganda baada ya kukaa muda mrefu bila kutumika.
Saruji zikiwa zimehifadhiwa katika hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Tarime zilizoganda baada ya kukaa muda mrefu zaidi ya miezi 10 bila kutumika
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime Simion Samwel akionyesha Saruji zilivyoganda zilizohifadhiwa shule ya msingi Murito
Saruji na vifaa mbalimbali vikiwa vimehifadhiwa kwenye chumba kinachotumiwa na wanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Murito kata ya Kemambo
Saruji na vifaa vilivyohifadhiwa kwenye zahanati tarajiwa ya Itandura kijiji cha Nyakunguru
Mwenyekiti wa kamati ya uchumi na ujenzi halmashauri ya wilaya Tarime ambaye pia ni Diwani kata ya Matongo -Nyamongo akijaribu kuvunja tofari, matofari hayo yanaelezwa kutengenezwa chini ya kiwango ambapo tofari moja linauzwa sh 2500 yanayojenga zahanati ya Itandura
Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi ya kijiji cha Nyakunguru akionyesha tofari zinazodaiwa hazina ubora
Wa kwanza kulia mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Simion Samwel akiwa ameongozana na wenyeviti wa kamati ya uchumi,ujenzi na huduma za jamii pamoja na wajumbe wa kamati ya ujenzi kijiji Cha Nyamwaga wakati wakutembelea ujenzi wa baadhi ya wodi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments