TIC YAFANIKIWA KUSAJILI MIRADI MIPYA 51 JANUARI HADI MACHI 2021

 Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho Dkt. Maduhu Kazi

Na Dickson Billikwija 

Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kimesema katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi mwaka 2021 kimefanikiwa kusajili jumla ya miradi mipya 51 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 451 huku kikibainisha sekta ya viwanda kuongoza katika miradi hiyo kwa kuwa na miradi 30 sawa na asilimia 59 ya miradi yote.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho Dkt. Maduhu Kazi wakati wa utoaji wa taarifa ya robo tatu mwaka 2020/2021 kwa waandishi wa habari.

Dkt. Kazi amesema miradi hiyo inatarajia kuzalisha ajira mpya 4,272 sawa na ongezeko la asilimia 3.5 ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka jana ambapo miradi 54 ilisajiliwa ambyo ilitarajiwa kuwekeza mtaji wa dola za kimarekani 283 milioni iliyozalisha ajira 4,127.

"Sekta iliyoongoza kwa uzalishaji wa ajira mpya ni utalii ambapo inategemea kuzalisha ajira 572 sawa na asilimia 13.4 ya ajira zote,"amesema Dkt. Kazi.

Amebainisha kuwa kati ya miradi 51 iliyosajiliwa mwaka huu miradi 13 sawa na asilimia 25 ni miradi ya wawekezaji wa ndani,miradi 26 sawa na asilimia 51 ni miradi ya wawekezaji wa kigeni,na kusisitiza miradi 12 sawa na asilimia 24 ni miradi ya ubia kati ya watanzania na wageni.

Aidha amesema TIC kinatunza kumbukumbu za miradi ya uwekezaji iliyosajiliwa hivyo wawekezaji ambao wamewekeza nchini bila kupitia kituo hicho hawako katika takwimu hizo  badala yake wawekezaji wengine husajiliwa na EPZA,Tume ya Madini na wengine huwekeza bila kupitia katika taasisi hizo.

Ameongeza kuwa katika kuendelea kuboresha uwekezaji nchini kituo hicho kimejiwekea mikakati mbalimbali ikiwemo kuendelea kuboresha mfumo wa kusajili miradi unaotumiwa na kituo hicho,kuunganisha Mfumo wa Kusajili Miradi (TIW) unaotumika na TIC na mifumo mingine inayohudumia wawekezaji nchini.

Mikakati mingine ni kuhamasisha zaidi uwekezaji kwa wazawa na ubia,kufuatilia kwa karibu wawekezaji kwa lengo la kung'amua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa miradi yao,pamoja na kuboresha zaidi matumizi ya tehama katika shughuli zote za kunadi na kuhumia wawekezaji.

Aidha ameongeza kuwa kituo hicho  miongoni mwa miradi iliyosajiliwa mwezi Aprili mwaka 2020 ni Mradi wa Kiwanda Kikubwa cha Mbolea cha Kampuni ya Itracom Fertilizers unaojengwa Dodoma utakaowekeza dola za Marekani milioni 180 na kuzalisha ajira za moja kwa moja milioni 3000 ambapo tani za mbolea 500,000.

Dkt.  Kazi alisema kituo hicho kinaendelea kuwakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza nchini kwani mazingira ya uwekezaji yameboreshwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments