MAREKANI YAAHIDI KUINUA SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI NCHINI


Na Mbaraka Kambona,
SERIKALI ya Marekani imesema itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuinua Sekta za Mifugo na Uvuvi ili ziweze kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa.


Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki wakati akizungumza na Waandishi wa Habari muda mfupi baada ya mazungumzo na Balozi wa Marekani Nchini Tanzania, Dkt. Donald Wright yaliyofanyika jijini Dodoma Aprili 14, 2021.

Ndaki alisema kuwa katika mazungumzo yao, Balozi  Wright alimuhakikishia kuwa Serikali ya Marekani ipo tayari kuleta wawekezaji kutoka Marekani ili kusisimua na kukuza sekta hizo mbili ili ziweze kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa viwanda.

“Balozi Wright ameahidi kuleta wataalamu kutoka marekani ili kubadilishana uzoefu wa kiufundi katika sekta ya mifugo ili wafugaji wetu waweze kubadilika na kuanza kufuga kibiashara ili  kukuza kipato chao na kuongeza ajira nchini,”alisema Ndaki.

Kuhusu uchumi wa Bluu ambao Serikali ya Tanzania imeanza kuwekeza, Ndaki alisema kuwa Serikali ya Marekani italeta wawekezaji kuja kuwekeza katika eneo hilo na kuisaidia Tanzania kuona tija ya uwekezaji  uchumi huo.

“Wenzetu wa Marekani wameendelea na wamewekeza sana katika uchumi wa bluu hivyo kupitia wao wanaweza kutusaidia kuimarisha eneo hilo ili sekta ya uvuvi iweze kuwa na tija zaidi kwa taifa letu,”aliongeza Ndaki

Aliendelea kusema kuwa Serikali ya Marekani ipo tayari kusaidia mapambano ya uvuvi haramu nchini ili kuhakikisha unakwisha na watu wanafanya uvuvi endelevu.

Aidha, Ndaki alimuomba Balozi huyo kuona uwezekano wa kuwapatia Watanzania nafasi ya kwenda kujifunza na kupata ujuzi kuhusu masuala ya mifugo na uvuvi katika nchi ya Marekani ili waweze kusaidia kuimarisha sekta hizo nchini.

Waziri Ndaki alisema kuwa ziara ya Balozi Wright ni kwa ajili kuimarisha ushirikiano katika sekta za mifugo na uvuvi, pia ililenga kutoa salamu za pole kutoka nchini Marekani kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.  Samia Suluhu Hassan baada ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kufariki.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments