MALARIA BADO TISHIO KWA WATOTO SINGIDA



Bango lililobeba Kaulimbiu ya Siku ya Malaria Duniani mwaka huu likiwa mbele ya moja ya majengo ya Kituo cha Afya Sokoine mjini Singida

 Na Abby Nkungu, Singida

 

IMEBAINIKA kuwa malaria bado ni tatizo kubwa linalosumbua watoto mkoani Singida kutokana na takwimu za idara ya afya kuonesha kuwa zaidi ya asilimia 30 ya wanaougua ugonjwa huo na kwenda kupatiwa matibabu kwenye vituo vya huduma wana umri chini ya miaka mitano.

Hayo yalibainika juzi Aprili 25 mwaka huu Tanzania ilipoungana na Nchi nyingine Wanachama wa  Shirika la  Afya Duniani (WHO)  kuadhimisha Siku ya Malaria Duniani chini ya kauli mbiu “Ziro Malaria inaanza na mimi–Nachukua hatua kuitokomeza”  

Taarifa ya idara ya afya  iliyotolewa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa  wa Singida, Dk Ernest Mugeta inaonesha kuwa kati ya wagonjwa 42,262 waliougua malaria kwa kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka jana na kwenda  kutibiwa vituo mbalimbali vya huduma, 10,469 walikuwa ni watoto ambayo ni sawa na asilimia 33.

"Katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, jumla ya watu 7,272 waliugua malaria na kwenda kutibiwa kwenye vituo mbalimbali vya huduma ambapo 2,581 sawa na  asilimia 35.5 walikuwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano", alifafanua Dk Mugeta.  

Aidha, alitaja baadhi ya  sababu zinazochangia watoto kuendelea kusumbuliwa na malaria kuwa ni pamoja na  kinga  yao  ya mwili kuwa chini; hivyo kuwa rahisi zaidi kushambuliwa na ugonjwa huo na wazazi au walezi kutotumia ipasavyo vyandarua katika kuwakinga watoto wao dhidi ya mbu.

Hata hivyo, alisema kuwa Mkoa umeweka mikakati mbalimbali ya kutokomeza ugonjwa huo wa malaria, ikiwa ni pamoja na kuhimiza matumizi ya vyandarua vyenye viuatilifu na kuangamiza mazalia ya mbu.

“Kwa mwaka 2020 tumeweza kugawa vyandarua 817,151 ngazi ya kaya kwa halmashauri za Ikungi, Iramba, Itigi, Manyoni na Mkalama na huduma ya chandarua Kliniki kwa wajawazito hudhurio la kwanza na watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja kwa kupata chanjo ya Surua/Rubella (MR 1) kwenye vituo huduma”, alieleza Dk Mugeta.

Akinamama mbalimbali walisema kuwa pamoja na juhudi hizo  za Serikali, bado kuna changamoto ya elimu juu ya umuhimu wa matumizi ya chandarua  katika jamii pamoja na  imani  potofu.

“Kweli vyandarua watu wanapewa lakini ukienda  vijijini utakuta vingi vimezungushiwa kwenye uzio wa kufugia kuku au bustani za mboga. Baadhi wanadai  vinapunguza  nguvu za kiume na wengine eti wanaona ni sawa na kujifunika sanda”, alisema mama Rose Ntandu.

Mwito  wao kwa wataalamu wa afya na wadau  wengine  wa mapambano dhidi ya Malaria ni kuendelea kutoa elimu zaidi kwa jamii juu ya umuhimu wa kutumia chandarua na madhara yanayoweza kujitokeza iwapo wataugua malaria; hasa watoto walio chini ya miaka mitano. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments