Waziri Mkuu Awatoa Hofu Wawekezaji Nchini


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewatoa hofu wawekezaji wanaozalisha bidhaa mbalimbali nchini baada ya kuwaeleza kuwa Serikali itahakikisha inawalinda na kulinda bidhaa zao ili waweze kupata masoko hapa nchini na hata nje ya nchi.

Ameyasema hayo leo (Jumanne, Aprili 27, 2021) alipotembelea kiwanda cha kuunganisha mabasi cha BM Motors kinachomilikiwa na Mtanzania Bw. Jonas Nyagawa na kiwanda cha madawa cha Kairuki, vilivyopo Kibaha mkoani Pwani. Amesema ameridhishwa na uwekezaji huo.

Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa lengo la kuinufaisha nchi pamoja na muwekezaji. Hivyo, ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali.

“Serikali tupo na nyie, maamuzi tuliyofanya ya kuweka mazingira wezeshi ni maamuzi sahihi, tutapita kusikia changamoto za kila mmoja wenu na tutazitatua, ongezeni mitaji kwenye uwekezaji wenu, tumieni taasisi za fedha kuongeza mitaji”.

“Tumeondoa usumbufu katika ulipaji kodi, tumewataka TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) watumie njia sahihi na rafiki ya ukusanyaji kodi. Ujenzi wa viwanda ni njia tuliyoiweka sisi Serikali ya kutatua changamoto ya ajira”.

Pia, Waziri Mkuu ameziagiza taasisi zote za Serikali zinazohusika na masuala ya uwekezaji zihakikishe wawekezaji wote walioonesha nia ya kuwekeza nchini wanasaidiwa na kufanikisha mchakato huo bila ya usumbufu wa aina yoyote.

“Taasisi zote zinazohusiana na uwekezaji zihakikishe kila ambako panatamaniwa na muwekezaji huduma muhimu zipatikane iwe maji, umeme barabara na hata viwanja vipatikane kwa urahisi”.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi wa Mji Kibaha Bibi Jenifa Omolo atumie vyombo vya habari alitangaze eneo la uwekezaji la Zegereni lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda. “…Wakuu wa idara waondoe urasimu ili watu waje kuwekeza katika eneo hili”.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo aliwahakikishia wawekezaji ambao wanataka kuwekza katika eneo la viwanda la Zegereni kuwa changamoto zote katika eneo hilo ikiwemo maji, umeme na barabara zitatatuliwa.

Baada ya kutembelea kiwanda cha kuunganisha mabasi, Mheshimiwa Majaliwa alitembelea kiwanda cha madawa cha Kairuki kilichopo katika eneo hilo la Zegereni ambacho kinatarajiwa kuanza uzalishaji Juni, 2021.

Waziri Mkuu amewahamasisha wawekezaji kujenge viwanda vya kuzalisha dawa kwa kuwa soko lipo katika hospitali, vituo vya afya na zahanati. Kiwanda hicho kitazalisha dawa za maji, tiba, analgesics na antibiotics.

Gharama ya uwekezaji wa kiwanda hicho ni shilingi bilioni 45 na kitakuwa na uwezo wa kuzalisha chupa za dripu milioni 55 kwa mwaka, ambapo 60% ni kwa ajili ya soko la ndani na 40% ni soko la nje, kwa kuanzia watazalisha aina tisa za dawa za dripu.

(Mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments