JESHI LA MAGEREZA TARIME LAZIDI KUBUNI MIRADI ILI KUJITEGEMEA KIUCHUMI KATIKA KUWAHUDUMIA WAFUNGWA NA MAHABUSU

Na Dinna Maningo,Tarime.

JESHI la Magereza wilaya ya Tarime mkoa wa Mara linaendelea na utekelezaji wa shughuli za kiuchumi kwa kubuni miradi mbalimbali kwa ajili ya kujitegemea ili kuwawezesha wafungwa na mahabusu kupata chakula cha kutosha.

Akizungumza na Malunde 1 blog ofisini kwake, Mkuu wa Gereza la wilaya ya Tarime ASP Sebastian Dionis aliyehamishiwa wilaya hiyo Machi, 20,2021 akitokea gereza la wilaya ya Chato-Geita alisema kuwa tayari wameanza rasmi kulima zao la mahindi ekali 20 katika mlima Nkongoro kata ya Kitare.

Alisema mlima wa Nkongore ni eneo lililokuwa likitumiwa na baadhi ya wananchi kulima kilimo cha bangi na hivyo serikali kulikabidhi kwa Jeshi la Magereza mwaka 2017 kwa ajili ya shughuli za kilimo. 

"Eneo hilo lina ukubwa wa ekari 150 kati ya hizo ekali 20 tumelima mahindi eneo jingine tuko kwenye maandalizi ya kilimo cha kahawa,mlima huo wa Nkongore baadhi ya wananchi waliutumia kulima bangi.

"Hali iliyopelekea serikali kulichukua eneo hilo na kuwakabidhi jeshi la Magereza,kilimo kitasaidia kuwezesha wafungwa na mahabusu kupata chakula istoshe tulikuwa hatuna eneo la kilimo tunalima mahindi kwenye eneo la kuazima kutoka katika Jeshi la JWTZ -Nyandoto lenye ekali 30", alisema Dionis.


Mkuu huyo wa magereza alisema kuwa mbali na kujishughulisha na kilimo jeshi hilo limekuwa likiendelea kubuni miradi mbalimbali ambapo lina mradi wa zahanati ya afya inayotoa huduma ya jamii ndani ya magereza na nje ya magereza,kufanya usafi katika hospitali ya wilaya.

Miradi mingine ni huduma ya Bima ya afya na ushauri nasaha,hoteli,huduma ya vinywaji (Bar) duka la magereza, Bucha ya kuuza nyama ya ng'ombe, bustani ya mbogamboga, uchomeleaji wa vyuma kwa kutengeneza madirisha,vitanda na milango, utengenezaji wa majiko ya kupikia na ujenzi. 

"Bado tutaendelea kubuni miradi mingine tunajihusisha na ujenzi kupitia mafundi ambao ni wafungwa katika gereza letu, tunawaomba wananchi watuchangie miradi yetu ili tupate fedha ambazo zitasaidia kufanikisha huduma za magereza ikiwa ni pamoja na kutupatia kazi za ujenzi tuna mafundi wa kutosha ambao ni wataalamu katika ujenzi watakujengea mradi wako na utakamilika kwa wakati ,uchomeleaji wa vifaa na miradi mingineyo",alisema.

Dionis alisema kuwa magereza ya wilaya ya Tarime linahudumia wafungwa na mahabusu wapatao 512 kati ya hao wafungwa ni 112 na mahabusu 400 na kwamba miradi hiyo imekuwa inasaidia kuendesha shughuli za magereza na kujitegemea kiuchumi hivyo anawakaribisha wananchi kununua bidhaa za magereza na kupata huduma ya afya.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments