UN YAITAJA SIKU YA JANA KUWA MBAYA ZAIDI MYANMAR BAADA YA MAPINDUZI YA JESHI, RAIA 38 WAPIGWA RISASI


Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Myanmar ametangaza kuwa Jumatano ya jana ilikuwa siku mbaya na ya umwagaji mkubwa zaidi wa damu nchini humo baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa madarakani serikali ya kiraia tarehe Mosi Februari mwaka huu.

Christine Schraner Burgener amesema hayo baada ya jeshi la Myanmar kuua waandamanaji wasiopungua 38 wanaopinga mapinduzi ya jeshi jana Jumatano pekee.

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa amesema, mpaka sasa watu zaidi ya 50 wameuawa kwa kupigwa risasi na wengine wengi wamejeruhiwa tangu baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mapema mwezi uliopita nchini Myanmar.

Jeshi la Myanmar limewafyatulia risasi hai waandamanaji hao siku moja tu baada ya nchi jirani kutoa wito wa utulivu na kutangaza kuwa, ziko tayari kusaidia juhudi za kutafuta suluhisho la mgogoro wa nchi hiyo.

Tarehe Mosi mwezi wa Februari jeshi la Myanmar lilitwaa madaraka ya nchi baada ya kumkamata Rais wa nchi hiyo, Win Myint na viongozi wengine akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi mkubwa, kufuatia siku kadhaa za mivutano nchini humo. Jeshi la Myanmar pia limetangaza hali ya hatari ya kipindi cha mwaka mmoja na kukomesha utawala wa kiraia uliotawala nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 10.

Tangu wakati huo mamilioni ya Wamyanmari wamekuwa wakifanya migomo na maandamano ya nchi nzima wakipinga hatua ya jeshi ya kutwaa madaraka ya nchi.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post