CUF YAMLILIA RAIS MAGUFULI

Marehemu Rais Dkt John Pombe Magufuli enzi za Uhai wake.

**
Mimi binafsi na CUF- Chama Cha Wananchi tumepokea kwa masikitiko makubwa Taarifa ya Kifo cha Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea jana Machi 17, 2021 saa 12:00 jioni kutokana na maradhi ya moyo. Kwa hakika Taifa limegubikwa na huzuni kubwa na giza nene.


Masikio yamepokea taarifa ambayo akili haziko tayari kuibeba wala kuikubali kwa kuzingatia uhalisia kwamba ni wiki tatu tu zilizopita marehemu Rais Magufuli alifanya kazi kubwa bila kuchoka, za kuzindua miradi mikubwa ya Maendeleo ikiwa ni pamoja na Daraja la Ubungo ( Kijazi Interchange) na Stand Mpya ya mabasi iliyopo Mbezi, Dar es Salaam. Tunamuomba Mwenyezi Mungu ampe Pumziko la Amani.

Nakumbuka nilionana naye mara ya mwisho ana kwa ana nilipohudhuria Maadhimisho ya Siku ya Mahakama Dodoma tarehe 01 Februari 2021. Alinikaribisha bila mimi kutarajia nizungumze maneno machache kwenye hafla hiyo. Nilimkumbusha ahadi zake alizotoa mwaka 2015 alipokuwa anazindua Bunge la 11 ikiwa ni pamoja na kukamilisha upatikanaji wa Katiba Mpya.

Pia nikaeleza kuwa katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge la 12 aliwagawia Wabunge hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge la 11 mwaka 2015 na akasisitiza kwamba yote ambayo hayakutekelezwa katika kipindi chake cha kwanza yatatekelezwe katika kipindi cha pili. Nilipoeleza kuwa wasaidizi wake wa karibu kama vile Profesa Palamagamba Kabudi na Humphrey Polepole walikuwa wajumbe wa Tume ya Jaji Warioba na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Rais Magufuli alinikumbusha kuwa Dr Tulia Ackson Naibu Spika pia alikuwa Mjumbe wa Bunge la Katiba.

Siku hiyo Marehemu alionekana ana afya njema na mchangamfu. Alinitania kwa kusema kuwa baada ya uchaguzi Prof. Lipumba amenenepa. Aliupokea ujumbe wangu vizuri. Niliamini kabisa kiporo cha upatikanaji wa Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi atakifanyia kazi kwa dhati katika kipindi chake cha pili. Hasa ukizingatia kwamba mara kwa mara alisisitiza kwamba hiki kingekuwa kipindi chake cha mwisho cha uongozi wake kama Katiba ya nchi inavyoelekeza.

Kifo chake cha ghafla kinatia uchungu na simanzi kubwa. Amri ya Mungu haina makosa. Kila wakati kauli za Rais Magufuli zilimtanguliza Mwenyezi Mungu.
Watanzania tutamkumbuka marehemu Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwa makubwa aliyoyafanya kwenye ujenzi wa miundombinu, kupambana na ufisadi kwa kiwango kikubwa kuliko wakati wowote katika historia ya nchi yetu na kuimarisha utendaji na uwajibikaji wa watumishi wa serikali.

CUF- Chama Cha Wananchi kinatoa Salamu za Pole na Rambirambi kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, familia ya marehemu na Watanzania wote kwa ujumla kufuatia msiba huu mzito. Kwa hakika tumebaki wakiwa na ni vigumu kulizoea pigo hili la kwanza la aina yake. Pamoja na kuwapoteza Marais wastaafu, hii ni mara ya kwanza kwa Jamhuri ya Muungano, kumpoteza Rais akiwa madarakani.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe subira njema na utulivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huu mkubwa.

Kwa kuzingatia Katiba ya nchi hususan Ibara ya 37 (5) Mama Samia Suluhu Hassan ndiye atakayeapishwa kuwa Rais wa sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu, utekelezaji mwema na wa haki wa majukumu yake utakaoliletea maendeleo na heshima Taifa letu na kuenzi Haki, Umoja na Mshikamano wa Kitaifa kwa kiwango cha juu kuliko nyakati zote. Bila shaka ahadi za Rais Magufuli ikiwa pamoja na kukamilisha mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi itatekelezwa na Rais mpya Mama Samia Suluhu Hassan.

Chama cha CUF kinaungana na Watanzania wote katika msiba huu mkubwa. Bendera za Chama cha CUF, Ofisi zote za Chama Tanzania Bara na Zanzibar zitapepea nusu mlingoti kwa siku 14 za maombolezo. Vikao vya Chama vya Kitaifa vilivyopangwa kuanza tarehe 20 -25 Machi 2021 vimeairishwa mpaka itakapotangazwa baadaye baada ya siku 14 za maombolezo.


Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe milele. Amina.


HAKI SAWA KWA WOTE


Prof. Ibrahim Lipumba
Mwenyekiti- Taifa
CUF- Chama Cha Wananchi
Machi 18, 2021

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments