KATIBA YA TANZANIA INAVYOELEZA BAADA YA RAIS KUFARIKI DUNIA


Makamu wa Rais ,Samia Suluhu Hassan
**
Baada ya Rais wa Tanzania John Magufuli kufariki dunia, hakuna uchaguzi mwingine unaofanyika badala yake, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ataapishwa kuwa Rais kwa kipindi kilichosalia katika muhula wa miaka mitano.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 37 (5), baada ya Samia kuapishwa atashauriana na chama anachotoka (CCM) kisha atamteua mtu atakayekuwa makamu wa Rais.

Katiba

37 (5) Endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais
kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu
 kazi zake kutokana na maradhi ya mwili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za Rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano na kwa masharti yaliyoelezwa katika ibara ya 40, kisha baada ya kushauriana na chama cha siasa anachotoka Rais atapendekeza jina la mtu atakayekuwa Makamu wa Rais na uteuzi huo utathibitishwa na Bunge kwa kura zisizopungua asilimia hamsini ya Wabunge wote.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli amefariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa akipatiwa matibabu.

Taarifa za kifo cha Rais Magufuli, zilitangazwa jana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ametangaza kifo akisema Magufuli alifariki dunia saa 12 jioni kwa maradhi ya moyo baada ya kulazwa katika hospitali hiyo tangu Machi 6.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments