RAIS WA KENYA UHURU KENYATTA ATANGAZA SIKU 7 ZA MAOMBOLEO KUFUATIA KIFO CHA RAIS MAGUFULI

Rais Kenyatta (kulia) na Rais Magufuli (kushoto)
***

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameomboleza Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli akisema Magufuli ni mtoto wa Afrika hivyo kifo chake ni pigo kubwa.

Rais Kenyatta ametuma salamu za rambirambi kwa Watanzania akiwemo mkewe Janeth Magufuli kutokana na kifo hicho.

Kama heshima kwa kiongozi huyo wa nchi jirani, Rais Kenyatta amesema Kenya itamuomboleza kwa siku saba.

Rais ameagiza pia bendera ya Kenya pamoja na ile ya jumuia ya Afrika Mashariki kupepea nusu mlingoti hadi wakati atakapozikwa kiongozi huyo.

Amemsifu Magufuli kama kiongozi aliyeitetea Afrika tangu achukue hatamu za uongozi wa Tanzania 2015 alipochaguliwa kwa tiketi ya CCM.

"Bendera ya Kenya na ile ya Jumuiya ya Afrika Mashariki itapepea nusu mlingoti kuanzia leo hadi kuzikwa kwake," amesema Kenyatta.

Rais amesema tayari amezungumza na makamu wa rais Tanzania Samia Suluhu na kumhakikishia kuwa Kenya itasimama na nchi hiyo.

Alikumbuka kipindi cha uongozi wake na Magufuli akiwamo ziara yake rasmi ya Kwanza humu nchini.

"Alikuja tukafungua mradi wa barabara na baadaye akanipa heshima kubwa kusema anataka kumuona Mama Ngina na akaenda kumtembelea," Rais amesema.

Kifo cha Magufuli kilitangazwa rasmi na Makamu wake Samia Suluhu Jumatano usiku na kusema Tanzania itaomboleza kwa siku 14. Samia alisema Magufuli alifariki Jumatano MachI 17 saa kumi na mbili JIONI wakati akipokea matibabu ya moyo jijini Dar es salaam.

Ni kifo ambacho kimeitikisa Afrika kwani Rais huyo aliitetea Afrika na ajenda zake.

Via Tuko News

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments