AANGUKA NA KUFARIKI DUNIA AKIOMBOLEZA KIFO CHA MKE WAKE


Jamaa aliyetambuliwa kwa jina Daniel Tauni kutoka Navakholo, Kakamega nchini Kenya mnamo Ijumaa, Machi 19,2021 alizimia na kisha baadaye akatangazwa ameaga dunia akimuomboleza mkewe.

 Tauni mwenye umri wa miaka hamsini na tano alikuwa amepanda kwenye jukwaa kumuomboleza mkewe, Janet Koikoi, wakati alipoanguka ghafla.

Alikimbizwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Navakholo ambapo muda mfupi baada ya kulazwa alitangazwa kuwa amefariki dunia kulingana ripoti ya K24. 

Ripoti kutoka kwa jamaa zake, Wilson Maike na Nuru Namsonge, zinaonyesha kuwa mkewe alifariki dunia baada ya kuugua Kifua Kikuu wiki iliyopita. 

Mwili wa Tauni ulihamishiwa hadi makafani ya Hospitali ya Kaunti ya Webuye ambapo utahifadhiwa huku maandalizi ya mazishi yakifanywa.

Mazishi ya Janet, hata hivyo, yaliendelea japo kwa huzuni kubwa kutokana na yaliyotokea.

 Familia yake ilisema kwamba Tauni hakuwa na historia yoyote ya matatizo ya moyo. Hadi wakati wa chapisho la taarifa hii haikuwa imebainika kilichomuua marehemu. 

Kifo chake kinaongeza idadi ya watu walioanguka na kufariki dunia ghafla ambapo wengi wanahofia huenda iwaka ni matatizo yanayotokana na virusi vya corona.

Mnamo Julai 2020, watu watatu waliripotiwa kuzirai na kufariki dunia ghafla katika kaunti za Makueni, Nairobi na Mombasa. 

Katika kisa cha kwanza kilichotokea katika kijiji cha Kitivo Makueni, mzee mmoja alifariki dunia ghafla baada ya kushindwa kupumua kwa kile maafisa wa afya walisema ilikuwa Covid-19.

 Wengine wawili pia walilalamika maumivu ya kifua kabla ya kuanguka na kufariki dunia ghafla.

CHANZO TUKO NEWS

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments