EWURA YAITAKA SUWASA KUONGEZA VYANZO VIPYA VYA MAJI


Wajumbe wa Bodi ya Ewura na Menejimenti ya Ewura wakikagua Chanzo kikuu cha maji Mwankoko, nje kidogo ya mji, wakiwa katika ziara yao ya siku moja mkoani Singida
**
Na Abby Nkungu, Singida

MAMLAKA ya kudhibiti bidhaa za nishati, maji na gesi asilia (Ewura) imeitaka Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Singida mjini (Suwasa) kuongeza vyanzo vingine vipya vya maji ili kukidhi mahitaji halisi ya wakazi zaidi ya 184,500 waishio Manispaa ya Singida.

Mwito huo ulitolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ewura, Fadhili Manongi alipokuwa kwenye ziara mkoani hapa na Bodi yake pamoja na Menejimenti ili kukagua miradi ya maji, kusikia changamoto zinazoikabili Suwasa na kushauri namna bora ya kuzitatua.

"Kutokana na mahitaji ya maji kuwa makubwa katika Manispaa ya Singida kuliko uzalishaji, kuna haja mkaanza kutafuta vyanzo vingine vipya vya maji ili kukidhi matarajio ya wakazi wote katika suala zima la upatikanaji maji safi na salama" alisema na kuongeza;

Lakini, pia ebu tumieni kikamilifu uwezo mdogo wa uzalishaji maji uliopo. Pia, lindeni vyanzo vichache vilivyopo kwa kushirikiana na wadau wote".

Aidha, alielekeza Mamlaka hiyo kubadilisha dira zote za zamani ambazo uwezo wake wa kusoma kwa usahihi matumizi ya maji umepungua badala yake waweke nyingine mpya ili kupunguza au kuondoa kabisa manung'uniko ya wateja yasiyo ya lazima.

Akizungumzia uwezo mdogo wa kifedha, aliishauri Suwasa kuingia ubia na wawekezaji binafsi ili kuinua uwezo wake kimapato, iwapo Sera inaruhusu huku akisisitiza umuhimu wa kuweka Mtandao wa majitaka akisema kuwa ukuaji wa mji wa Singida hautawasubiri Suwasa.

"Ebu kuweni wabunifu, Singida hakuna kiwanda cha kutengeneza maji ya kunywa ya chupa. Kwa nini hiyo isiwe fursa mojawapo ya nyie kujiongezea mapato?" alihoji Mwenyekiti huyo.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Geoffrey Chibulunje alishauri Suwasa kujipatia nishati mbadala kuendeshea mitambo yake ya maji huku akitahadharisha juu ya kuitegemea sana Tanesco.

Awali, akiwasilisha taarifa ya SUWASA ya huduma ya maji Manispaa ya Singida na Miji ya Itigi na Manyoni, Fatina Mmbaga alieleza kuwa wastani wa uzalishaji maji wa Mamlaka hiyo kwa Manispaa ni mita za ujazo 8,426 tu kwa siku; sawa na asilimia 58 tu ya mahitaji halisi ya mita za ujazo 14,410.

Alitaja baadhi ya changamoto kuwa ni gharama kubwa za nishati ya umeme ambapo Mamlaka hiyo hulazimika kulipa wastani wa Sh milioni 70 kila mwezi kwa ajili ya uendeshaji wa mitambo yake huku akibainisha kuwa hadi Februari 15 mwaka huu Mamlaka hiyo inadai zaidi ya Sh milioni 335 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post