TAKUKURU YAREJESHA MIL.176.5 NA NYUMBA MOJA YA MIKOPO UMIZA KWA WASTAAFU 17

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa [TAKUKURU]mkoa wa Dodoma imefanikiwa  kumpata  mmiliki wa kampuni Geneva  Credit Shop ya Mjini Kondoa  Abubakary Kinyuma  ama maarufu Bwana Mapesa na kumwamuru kurejesha Tsh.Milioni mia moja sabini na sita laki tano  sitini na tano elfu[176,565,000] na nyumba moja kwa walimu wastaafu  17.

Akizungumza na Waandishi wa habari  leo Februari  18,2021 jijini  Dodoma mkuu wa TAKUKURU mkoani Dodoma Sosthenes Kibwengo amesema uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya watumishi wa umma wilayani Kondoa wanapokaribia kustaafu  huchukua mikopo midogo  kwa Bw.Mapesa ambaye amekuwa akichukua kadi zao za benki na kuzihifadhi na pindi mafao yao yanapotoka hujitwalia kiasi kikubwa cha fedha  kwa riba kubwa  hadi kufikia   asilimia elfu kumi.

“Mwezi uliopita [Januari 2021 ]tuliwatangazia  kuwa tunafanya uchunguzi  dhidi ya kampuni ya ya Geneva  Credit  Shop  ya mjini Kondoa  inayojihusisha na ukopeshaji wa fedha ,baada ya kupokea malalamiko ya wananchi  wengi ambao wanadai kupatiwa mikopo umiza  na kampuni hiyo na uchunguzi wetu ulibaini kuwa  walilipishwa fedha hizo za mafao na kunyang’anywa   na Bw. Mapesa  kinyume na taratibu",amesema.

Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoa wa Dodoma amesema mwalimu mstaafu mmoja  alikopeshwa Tsh. Laki tatu na elfu hamsini [350,000/=] pamoja na kurejesha Tsh. Milioni nne na laki sita[4,600,000=/] pia alinyang’anywa nyumba yenye  yenye thamani ya Tsh.Milioni  thelathini na saba[37,000,000/=] iliyopo kiwanja  Namba  115 kitalu C   eneo la Ndachi East jijini Dodoma.

Bw.Kibwengo ameainisha baadhi ya malipo yaliyofanyika  leo kwa wastaafu ni pamoja na Juma  Hindo aliyerejeshewa   Tsh.Milioni ishirini na saba na laki nne  na  themanini na nane elfu[27,488,000/=],Ayub Bakari aliyepatiwa Milioni  ishirini na tatu na laki nne[23,800,000/=],Ally Tarimo  milioni kumi na nne laki moja na nusu[11,150,000/=],huku fedha zingine zilizorejeshwa ni   Tsh.milioni ishirini na tatu  na laki nne[23,400,000/=],  pamoja na Tsh.Milioni kumi na sita na laki nane[16,800,000/=].

Aidha,Bw.Kibwengo ameendelea kufafanua kuwa kwa kushirikiana na mamlaka ya mapato Tanzania[TRA] TAKUKURU inaendelea kukokotoa kiasi cha kodi ambacho kampuni hiyo ya ukopeshaji inadaiwa  na  kuendelea kufuatilia Tsh.Milioni mia moja themanini na nne  laki tano themanini na sita [184,586,000/=]za wakopeshwaji  22  ambazo pia zinapaswa kurejeshwa na BW.Mapesa.

Katika hatua nyingine Bw.Kibwengo amesema TAKUKURU imemrejeshea Bw.Dismas Kweka   ,mfanyabiashara na mkazi wa Nkuhungu jijini Dodoma  Tsh.milioni tano  [5,000,000/=],

“Ufuatiliaji wetu  umewezesha kuziokoa kutoka kwa Bw.Richard Mwambenje  ambapo Disemba 2021 tulimrejeshea Bw.Kweka  ambaye aliuziwa kiwanja Na.18   kwa Tsh. Milioni tisa na laki saba[9,700,000/=] na leo anapatiwa kilichosalia  kiwanja hicho kilitolewa na mwananchi mmoja kama sadaka  kwa Jumuiya ya Uamsho wa Wakristo  Tanzania [UWATA]  lakini Bw.Mwambenje ambaye alikuwa katibu wa UWATA alikiuza  kwa kutumia mkataba wa kughushi”amesema .

Pia,Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoani Dodoma Bw.Kibwengo amebainisha kuwa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma imefanikiwa kurejesha deni  la Tsh.milioni hamsini na moja  laki sita  sabini na nane elfu  na mia saba thelathini na tatu[51,678,733/=] kwa chama cha akiba na kukopa  cha Ufundi SACCOS  baada ya kuwabana wanachama  ambao ni wadaiwa sugu wa muda mrefu.

Hivyo,Bw.Kibwengo ametoa wito kwa wakopeshaji wa fedha mkoani Dodoma kuzingatia sheria ,kanuni na taratibu  za nchi na kuacha  na kuacha kuwatoza wananchi riba umiza huku pia akiwaasa wananchi kujihadhari na mikopo umiza  na kutokubali kukabidhi kadi zao za benki kwa mtu yeyote.

Kwa upande wao baadhi ya walimu wastaafu akiwemo Mwalimu Juma Hindo na Mwalimu Halima Tarimo wameipongeza TAKUKURU kwa kuendelea kutetea Wanyongo ambapo mwalimu Hingo amesema alikopa Tsh. Laki mbili baada ya kustaafu aliamuliwa kulipa  riba ya Tsh,milioni 30.

“Bado huyu ndugu yetu anazidi kuumiza wanyonge mwaka 2014 nikiwa kazini nilikopa Tsh.laki mbili baada ya kustaafu mwaka 2017 Mzee Mapesa alikuja na mgambo wake wawili walileta bili ya Tsh.Milioni 30 mimi sikuwa na pesa maana pesa zote zilikuwa benki na nilikuwa na trekta niliuza kwa Tsh.Milioni 16 na nikaenda benki kutoa milioni 14 Jumla nikampa milioni 30”,amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments