DKT. GWAJIMA AONGOZA HARAMBEE YA UJENZI WA WODI YA SARATANI - MWANZA.... BILIONI 1.3 ZAPATIKANA


Na. Catherine Sungura,WAMJW-Mwanza
Jumla ya shilingi bilioni 1.3 zimechangwa na wadau mbalimbali ili kufanikisha ujenzi wa wodi ya Saratani inayojengwa katika hospitali ya rufaa ya kanda-Bugando inayotarajia kukamilika mapema mwezi agosti mwaka huu.

Akiongea wakati wa harambee hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa BOT jijini Mwanza  kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima alisema fedha hizo zimegawanyika katika sehemu tatu ambazo ni vifaa, ahadi na fedha taslim.

Dkt. Gwajima alisema harambee hiyo imekuja wakati dunia ikiadhimisha siku ya Saratani duniani ambapo lengo kubwa ni kukumbushana na kuimarisha huduma za saratani ikiwa ni pamoja na kutimiza majukumu ya kila mmoja katika kudhibiti ugonjwa huo.

 “Tunapaswa kujiuliza kama mwananchi amechukua vipi majukumu katika kupambana na kutekeleza  mkakati kwa kuhakikisha amechunguzwa mapema ama kupata matibabu  mapema kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini”.Alihoji Dkt. Gwajima

Aidha, Waziri huyo aliwapongeza watumishi,wageni waalikwa na  wadau wa Mwanza kwa mchango huo ambao utasaidia hatua kubwa “najua kazi bado ni kubwa ila mwanzo ni hatua nyingine hivyo  bado tunahitaji  fedha kwani ujenzi huu ukikamilika utawanufaisha watu wengi kwenye mikoa 8 inayohudumiwa na hospitali hii hivyo ni jambo jema pia kwa Afrika Mashariki”.

Akitaja takwimu za Saratani hapa nchini Dkt. Gwajima alisema katika kila watu 100,000 kuna wagonjwa  76 wapya wa saratani, idadi ya vifo vinavyosababishwa  na ugonjwa wa saratani  ikifikia watu 68 kwa kila wagonjwa 100 na sehemu kubwa ya hali hiyo ya vifo inachangiwa  hasa na wagonjwa wengi kuchelewa kupata huduma  kwa wakati kutokana na sababu mbalimbali  hivyo kufika wakati wakiwa katika hatua za juu za ugonjwa huo ambapo matibabu huwa na matokeo yasiyo mazuri.

“Mwaka 2013, Wizara ilizindua Mpango Mkakati wa kwanza wa kudhibiti wa magonjwa ya saratani na ilipofika mwezi februari  mwaka 2019, Wizara ilizindua mwongozo wa huduma za saratani ili kuimarisha utoaji  wa huduma  bora za saratani  nchini.

Hata hivyo alisema  Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu  ya upatikanaji dawa  pamoja na uwepo wa wataalamu waliobobea katika kutibu  ugonjwa wa saratani, lengo likiwa ni kupunguza  idadi ya wagonjwa wapya wa vifo vitokanavyo na saratani angalau kwa asilimia 50 hadi ifikapo mwaka 2030.

Gharama za ujenzi huo wa ghorofa tatu umekadiriwa  kutumia shilingi bilioni 5.4 ambapo hospitali ilikusanya shilingi bilioni 1.3 na Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga shilingi bilioni moja kwenye ujenzi huo ambao utasaidia kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wakazi wa mikoa ya Mwanza, Simiyu, Geita, kagera, Tabora, Mara, Shinyanga. na Kigoma.
_MWisho-


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments