Tanzia : BALOZI JOHN KIJAZI AFARIKI DUNIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli anasikitika kutangaza kifo cha Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John William Kijazi kilichotokea leo Februari 17,2021 saa 3:10 usiku akiwa katika Hospitali ya Benjamini Mkapa Jijini Dodoma alikokuwa anapatiwa matibabu.

Rais Magufuli amesema taratibu za mazishi ya marehemu Balozi Kijazi zitatangazwa baadae.

Mungu amuweke mahali pema peponi. Amina.
Balozi Mhandisi John William Herbert Kijazi amekuwa mwakilishi wa Tanzania nchini India, Singapore, Sri Lanka, Bangladesh na Nepal mwenye makazi yake jijini New Delhi, India kuanzia mwaka 2007 - 2016 na hivyo kumfanya kuwa Mkuu wa Mabalozi wote wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi.

Kabla ya kuwa balozi, Mhandisi Kijazi alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na baadaye Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu kuanzia mwaka 2002 hadi 2006, baada ya kuteuliwa kuwa Balozi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na hatimaye kupangiwa kituo cha New Delhi, India.

Kati ya mwaka 1996 hadi 2002, Mhandisi Kijazi alikuwa Mhandisi Mwandamiziwa Ujenzi wa Barabara ndani ya Wizara ya Ujenzi kabla ya kupandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Barabara za Mikoa ndani ya wizara hiyo hiyo.

Balozi Mhandisi Kijazi alipata Shahada ya Sayansi ya Uhandisi wa Umma mwaka 1982 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye Shahada ya Uzamili katika Uhandisi wa Barabara Kuu kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza mwaka 1992.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments