TELEVISHENI YAFUNGIWA KWA KUKIUKA MWONGOZO WA UOMBOLEZAJI WA KIFO CHA MAALIM SEIF


Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar Omar Said

Na Haji Mtumwa - Mwananchi

 Tume ya Utangazaji Zanzibar imekifungia kituo cha televisheni cha Tifu kwa muda wa siku saba baada ya kudaiwa kurusha vipindi vinavyokwenda kinyume na uombolezaji wa msiba wa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Katibu Mtendaji wa tume hiyo, Omar Said akitoa taarifa hiyo alisema kwamba tume hiyo imelazimika kuchukua uamuzi huo baada ya kubaini kwamba kituo hicho katika kurusha wa vipindi vyake katika kipindi hiki, kinakwenda kinyume na muongozo uliotolewa na Serikali kupitia Tume hiyo.

Alisema kufuatia taarifa iliyotolewa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi hapo jana juu ya msiba wa Makamu wa kwanza wa Rais, Maalim Seif , tume hiyo ilitoa muongozo wa urushaji wa matangazo na vipindi kwa kipindi hiki cha muda wa siku saba za maombolezo kwa vituo vya televisheni, redio na mitandao ya kijamii.

Alisema katika muongozo huo wamevitaka vituo vyote kubadilisha ratiba zao za urushaji wa matangazo na vipindi, na kuandaa vipindi maalum vya maombolezo katika muda huu wa siku saba, huku wakiweka wazi kwamba hawatakuwa tayari kuona kuna kituo kinakwenda kinyume na muongozo huo.

Alisema licha ya hatua hiyo ya kutoa mwongozo kwa vituo hivyo, lakini kituo cha Tifu kimeonekana kwenda kinyume na muongozo huo, hivyo ililazimika kuchukuliwa hatua hiyo, ili kutoa fundisho juu ya kufuata muongozo wa serikali katika urushaji na uandaaji wa vipindi.

Via Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post