SIMBA SC WAIDUNGUA AS VITA KWAO DRCMabingwa wa Tanzania, Simba SC wameanza vyema hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, AS Vita Dimba la Mashahidi Jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo, Chriss Mugalu aliyeiadhibu timu ya nyumbani kwao kwa penalti dakika ya 61 baada ya beki wa AS Vita, Ousmane kuunawa mpira uliopigwa na kiungo Luis Miquissone, raia wa Msumbiji Goli la Simba katika mchezo huo uliopigwa Ijumaa usiku.

Simba walipata penati hiyo baada ya shambulizi kali lililofanywa na viungo Clatous Chama na Luis Miquissone ambalo lilizuiwa kwa mkono na beki wa Vita Ousmane Outtara katika eneo la hatari.

Ushindi wa Simba unakuja miaka miwili kamili toka walipofungwa goli 5-0 na AS Vita katika hatua ya makundi ya mashindano hayo msimu wa 2018/19. Hata hivyo Simba iliwafunga Vita 2-1 katika mchezo wa marudiano uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Simba ilionesha ukomavu na umakini wa hali ya juu katika safu ya ulinzi katika mchezo wa jana ikilinganishwa na kilichotokea jijini Kinshasa miaka miwili iliyopita. Kwa ujumla wake, Vita ilimiliki mchezo kwa asilimia 55 na kufanya mashambulizi mengi zaidi lakini safu ya ulinzi ya Simba iliweza kuhimili vishindo vya wapinzani wao.

Mechi ya jana ndio imefungua pazia la Kundi A na mchezo unaofuatia wa kundi hilo baina ya miamba ya Misri na mabingwa watetezi wa Klabu Bingwa Afrika Al Ahly na miamba ya Sudani Al-Merrikh utapigwa siku ya Jumanne jijini Cairo.

Simba imepata ushindi jijini Kinshasa miaka miwili baada ya kukubali kichapo cha 5-0 dhidi ya Vita.

Mchezo unaofuata kwa Simba utakuwa dhidi ya Al Ahly katika dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam mnamo Februari 23. 

Timu hizo mbili pia zilikutana katika hatua ya makundi msimu wa 2018/19 na mchezo wao wa mwisho Februari 12, 2019 Simba iliibuka na ushindi wa goli 1-0 jijini Dar es Salaam. Awali Simba ilikubali kichapo cha goli 5-0 jijini Cairo Februari 2, 2019.

Simba ina rekodi nzuri jijini Dar es Salaam toka msimu wa 2018/19 wa kutokupoteza mechi yoyote nyumbani na endapo wataandikisha ushindi dhidi ya Al Ahly watakuwa wamejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa hatua inayofuata ya robo fainali.

Jana pia umepigwa mchezo mmoja mwingine wa michuano hiyo wa kundi D baina ya Zamalek ya Misri na MC Alger ambao uliisha kwa sare ya 0-0 licha ya wenyeji Zamalek kuutawala mchezo huo kwa asilimia 76. Michezo mitano ya michuano hiyo ina inatarajiwa kupigwa hii leo.

Rekodi ya Simba Afrika
Simba inasifika kwa kuwa wakali nyumbani, na toka msimu wa 2018/2019 haijawahi kufungwa nyumbani katika michuano hiyo.

Alama zote 9 walizopata msimu wa 2018/19 na kufuzu kwenda robo fainali walizipata katika uga wa Mkapa.

Kutokana na rekodi hiyo ya Simba, ni dhahiri kuwa timu zote zitajikaza na kupambana zaidi watakapocheza jijini Dar es Salaam.

Endapo Simba itafuzu katika hatua ya makundi, itasonga mpaka hatua ya robo fainali. Hiyo ni hatua kubwa lakini si hatua kubwa zaidi kuwahi kufikiwa na Simba.

Simba imefika mara nne hatua ya robo fainali, mara ya mwisho ikiwa ni msimu wa 2018/19 ambapo walitolewa na miamba ya DRC TP Mazembe baada ya kukubali kipigo cha 4-1 mjini Lubumbashi.

Rekodi ya juu zaidi kwa Simba katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika ni hatua ya nusu fainali, ambayo walicheza mwaka 1974 ambapo ilibaki kidogo watinge fainali lakini walifungwa kwa mikwaju ya penati 3-0 na Ghazl Al-Mahalla ya Misri.

CHANZO- BBC SWAHILI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post