AMUUA MAMA YAKE MZAZI KWA KUMKATA SHINGO AONGEZE UTAJIRI


Jeshi la polisi mkoani Kagera linamshikilia Fredius Philibert Kibengo (38) mkazi wa kijiji cha Kibogoizi wilayani Karagwe kwa tuhuma za kumuua mama yeke mzazi kwa kumkata shingoni kwa kutumia kitu chenye ncha kali baada ya mganga wa kienyeji kumtaka kupeleka damu ya mama yake au ndugu yake wa karibu ili kutengenezewa dawa za kuongeza utajiri kwenye biashara.

Akizungumza leo Jumamosi Februari 20, 2021 Kamanda wa Polisi mkoani humo, Revocatus Malimi amesema tukio hilo limetokea Februari 18, 2021 saa 4 usiku ambapo Philbert alimuua mama yake aitwaye Lonsia Philbert (61) .

“Alimvamia mama yake usiku akiwa amelala na wajukuu zake watatu, akamkata shingo na kusababisha jeraha kubwa kisha akakimbia lakini kelele za watoto walioshuhudia tukio hilo ziliwashtua ndugu na majirani,” amesema Kamanda Malimi.

Amebainisha kuwa ndugu hao walitoa taarifa polisi walioanza msako na walimkamata Philbert wakati akiingia nyumbani kwake.

Ameeleza kuwa katika uchunguzi wa awali wamebaini kuwa alikufa baada ya kutoka damu nyingi huku akitaja tamaa ya kupata utajiri kuwa chanzo cha mauaji hayo.

Ameeleza kuwa katika uchunguzi uliofanywa na jeshi la polisi mkoani Kagera umebaini kuwa katika kipindi cha siku chache kabla ya tukio hilo kutokea mtuhumiwa alisafiri kuelekea nchini Burundi kutafuta dawa za kuongeza utajiri na aliporejea nyumbani kwake alimshirikisha mkewe kuhusu masharti aliyopewa na waganga wa kienyeji lakini mke wake hakukubaliana na masharti hayo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera Revocatus Malima amesema hata hivyo Februari 17 mwaka huu mtuhumiwa alionekana maeneo ya nyumbani kwa mama yake mzazi na ilipofika usiku wa kuamkia Februari 18,2021 alimvamia mama yake na kumkata na kitu chenye ncha kali kisha kupoteza maisha.

Hata hivyo Kamanda Malimi amewataka wakazi wa mkoa wa kagera kujiepusha na imani za kishirikina ambazo zimekuwa zikichangia mauaji ya wananchi wasio na hatia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments