ASKOFU EMMAUS MWAMAKULA AKAMATWA NA POLISI


Askofu Emmaus Mwamakula wa Kanisa la Uamsho la Moravian

Na Aurea Simtowe -Mwananchi
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia Askofu Emmaus Mwamakula wa Kanisa la Uamsho la Moravian kwa tuhuma za kuhamasiha maandamano nchi nzima kwa njia ya ujumbe wa maandishi aliotuma katika mitandao ya kijamii.

Taarifa ya kushikiliwa na polisi awali ilitolewa na Askofu huyo jana Januari 15, 2021 kupitia mtandao wa kijamiii na baadaye kuthibitishwa na Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Kupitia ujumbe wake alioandika mtandaoni jana Mwamakula alisema, “wapendwa Watanzania. Mimi Askofu Mwamakula nimechukuliwa nyumbani kwangu muda huu na watu wasiovaa uniform (sare) nimepelekwa kwa Kamanda wa kipolisi Mkoa wa Kinondoni. Mwanakondoo ameshinda tumfuate.”

Baadaye Jeshi la Polisi kupitia taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ilieleza kumshikilia askofu huyo.

Kupitia taarifa hiyo, Mambosasa alielezwa kuwa Mwamakula anashikiliwa kutokana na taarifa aliyoichapisha mtandaoni iliyokuwa ikihamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi kuandamana wakishinikiza na kudai Katiba Mpya, jambo ambalo ni kinyume na taratibu na sheria za nchi.

“Awali Jeshi la Polisi kupitia idara ya upelelezi Kanda Maalum Dar es salaam walifanikiwa kupata taarifa hiyo na kumkamata Askofu huyo kwa ajili mahojiano kwa jambo hilo ambalo lilileta taharuki kwa umma katika mitandao ya kijamii,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Mambosasa alitumia nafasi hiyo kutoa onyo “kwa yeyote ambaye ameshawishika na kupanga kuandamana, kuahirisha mara moja nia hiyo ovu ambayo iko kinyume na sheria.”

“Pia ifahamike ni kosa kufanya maandamano bila kuwa na kibali cha polisi ili kupewa ulinzi, na atakayejaribu kuandamana atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Mambosasa aliwataka wananchi wote wa Jiji la Dar es Salaam waendelee na shughuli zao za kukuza uchumi na kujipatia vipato vyao vya kila siku.

CHANZO - MWANANCHI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post