SERIKALI KUENDELEA KUTEKELEZA AHADI ZAKE UJENZI WA MELI ZIWA NYASA, MV MBEYA II YAANZA KAZI


 Na Grace Semfuko, MAELEZO
Katika kuhakikisha azma ya Serikali ya kuwa na miundombinu bora katika maziwa makuu ya Tanzania na inachangia katika kukua kwa uchumi wa nchi, Serikali ya awamu ya tano imeendelea utekelezaji wa ahadi zake za kuimarisha miundombinu hiyo ambapo katika Ziwa Nyasa sasa suala la usafirishaji limepatiwa ufumbuzi.

Wakati akilihutubia Bunge kwa mara ya kwanza mara baada ya kuchaguliwa na Watanzania kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 20, 2015 Rais Dkt John Pombe Magufuli alisema pamoja na mambo mengi ya kimaendeleo yatakayofanywa na Serikali yake lakini kuimarisha miundombinu na ujenzi wa uchumi ni miongoni mwa mambo ya kipaumbele.

“Masuala mengine tutakayoyawekea mkazo katika utawala wa Serikali ya awamu ya tano ambayo ninaamini yatasaidia katika kujenga uchumi wetu ni pamoja na masuala ya miundombinu, utekelezaji wa masuala haya yamefafanuliwa vizuri katika ilani ya CCM ya mwaka 2015 hivyo tutatekeleza ipasavtyo” alisema.

Miongoni mwa ahadi za Serikali ya awamu ya tano tangu ilipoingia madarakani ilikuwa ni kuimarisha sekta ya miundombinu pamoja na kuwahakikishia wakazi waishio kando ya Bahari na maziwa nchini usafiri salama na wa uhakika.

Wakazi waishio kando ya Ziwa Nyasa kwa muda mrefu walikuwa wakihitaji usafiri wa njia ya maji ambao sasa jawabu lake limepatikana kufuatia kukamilika kwa meli kubwa ya mizigo na abiria na kusababisha wakazi hao kuondokana na adha ya usafiri katika maeneo yao.

Iliwachukua mwendo wa muda mrefu wakazi wa maeneo hayo wanaohitaji kwenda kwenye mikoa ya Mbeya na maeneo mengine kuzunguka umbali mrefu kwa njia ya gari huku suluhisho la njia ya mkato kwenye ziwa hilo ikiwa inafanyiwa kazi.

Jumanne January 5, 2021 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alizindua rasmi Meli ya MV Mbeya II mara baada ya ujenzi wa meli hiyo kukamilika.

Meli hiyo mpya ya MV Mbeya II ni miongoni mwa ujenzi wa meli tatu za ambazo mbili kati yake  ni za mizigo ikiwepo MV Ruvuma na MV Njombe zote zikiwa ni za mizigo zinazogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 11 na hiyo moja iliyokamilika ya MV Mbeya II iliyogharimu shilingi Bilioni 9.1 za Kitanzania.

Pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa Meli hiyo mpya pia Serikali inaimarisha Bandari zilizopo kwenye ziwa hilo ikiwepo ujenzi wa Bandari ya Ndumbi

Ziwa Nyasa lenye jumla ya Bandari 15 kwa upande wa Tanzania zikiwepo sita za mkoani Ruvuma, Sita za Mkoani Njombe na tatu za Mkoani Mbeya limekuwa na tija ya kiuchumi kwa wananchi waishio kwenye mikoa hiyo ambapo sasa mpango wa Serikali ni kuhakikisha wananchi wananufaika zaidi.

Ujenzi wa Meli hiyo itakayokuwa ikifanya safari zake katika Ziwa Nyasa kutoka Bandari ya Kyela Mkoani Mbeya hadi Mbambabay Mkoani Ruvuma na kwenye maeneo ya nchi jirani za Malawi na Msumbiji  umegharimu shilingi Bilioni 9.1 za kitanzania na ina uwezo wa kubeba abiria 300 na tani 200 za mizigo.

Meli hiyo imejengwa na Kampuni ya Kitanzania ya Songoro Marine huku lengo la Serikali ni kuhakikisha kampuni za kitanzania zinanufaika katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya kijamii.

Lengo la ujenzi wa Meli hiyo pamoja na nyingine zitakazokuwa zikifanya kazi kwenye Ziwa Nyasa ni kuboresha uchumi wa wakazi wa maeneo hayo pamoja na Taifa kwa ujumla kupitia sekta ya usafirishaji.

Katika uzinduzi huo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Tanzania inapakana na nchi nane ambazo zinategemea kupata bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania na kuwataka wakazi nchini kutumia fursa ya meli hiyo kufanya biashara ili kujinufaisha kiuchumi.

Amesema kutokana na kuona umuhimu wa kuwajengea uwezo wananchi kiuchumi na ndio maana Serikali inaamua kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ikiwepo ujenzi wa Meli za kisasa za Abiria na Mizigo, ujenzi na ukarabati wa barabara, Ujenzi wa Bandari za kisasa pamoja na miundombinu ya reli lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma zote za kijamii.

Deusdedit Kakoko ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini Tanzania anasema kukamilika kwa ujenzi wa meli hiyo kunaendelea kuleta ufanisi katika utendaji kazi wa bandari huku akisema bado mamlaka inaendelea na uboreshaji wa bandari pamoja na ujenzi wa meli.

Ujenzi wa Meli katika Ziwa Nyasa unakwenda sambamba na uimarishwaji wa miundombinu ya barabara ambapo ujenzi wa barabara ya Mbinga-Mbambabay yenye urefu wa kilomita 66 iliyogharimu shilingi Bilioni 129.361 umekamilika ambapo wakazi wa maeneo hayo sasa wananufaika na matunda ya kazi hiyo iliyofanywa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema ujenzi wa barabara hiyo ni ndoto za Rais Magufuli za kuzidi kuimarisha miundombinu ya usafirishaji nchini na kwamba Wizara ya yake itahakikisha inasimamia kikamilifu bandari nchini katika kukusanya mapato kwa njia ya kielektroniki ili ziweze kujiendesha.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments