ZAIDI YA WATANZANIA MILIONI 12 WAISHIO VIJIJINI WAFIKIWA NA HUDUMA ZA MAWASILIANO


Na Celina Mwakabwale, UCSAF
Mtendaji Mkuu wa mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF), Justina Mashiba amesema mpaka sasa zaidi ya wananchi millioni 12 waishio maeneo ya vijijini na yasiyo na mvuto wa kibiashara pamoja na wale wa mipakani na kanda maalum wamefikiwa na huduma mbalimbali za mawasiliano ikiwemo simu, runinga, radio pamoja na mawasiliano ya posta.

Bi. Mashiba ameyasema hayo wakati wa ziara ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile aliyetembelea tasisisi hiyo na kufanya kikao na wajumbe wa bodi, menejimenti pamoja na wafanyakazi. Katika ziara hiyo aliambatana na Katibu Mkuu, Dkt. Zainab Chaula, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Jim Yohazi pamoja na baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo.

Dkt Ndugulile ameipongeza UCSAF kwa kufikisha huduma za mawasiliano kwenye maeneo mbalimbali nchini huku akiitaka kuwekeza zaidi katika teknolojia yenye gharama nafuu ili kuyafikia kwa haraka maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma za mawasiliano. Hivi sasa UCSAF inatumia shilingi milioni 350 kujenga mnara mmoja wa mawasiliano.

Ameongeza kwa kusema kuwa, sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya habari inabadilika kwa kasi hivyo ameitaka wizara kukamilisha uandwaaji wa sheria ya TEHAMA ili kuendana na kasi ya mabadiliko hayo.

Akizungumza na wajumbe wa bodi Dkt Ndugulile ameagiza kuwepo na utaratibu mzuri wa kufanya kazi kwa ukaribu na kwa ushirikiano kati ya Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) na UCSAF ili kuongeza kasi ya upelekaji wa huduma mbalimbali za mawasiliano katika maeneo wanayoshirikiana.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula ameipongeza UCSAF huku akiitaka kuendelea kufikisha huduma za mawasiliano ili kuendana na malengo ya kuanzishwa kwa wizara hiyo.

Hadi sasa mfuko wa mawasiliano kwa wote umefanikiwa kufikisha huduma mbalimbali za mawasiliano ikiwa ni pamoja na kuwasha minara katika kata 633 zenye vijiji 2,320, kuunganisha mtandao wa intaneti na kutoa vifaa vya TEHAMA kwa shule 711, kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu 2,213 wa shule za UMMA kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara pamoja na kujenga vituo 10 vya TEHAMA visiwani Zanzibar.

 Mfuko wa Mawasiliano Kwa Wote (UCSAF)


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post