WAMUOMBA RAIS MAGUFULI KUINGILIA KATI MRADI WA MAJI ULIOGHARIMU MIL.511 LAKINI WANANCHI HAWAPATI MAJI

Na Dinna Maningo,Tarime

WANANCHI wa Kata ya Nyakonga wamemuomba Rais John Magufuli kuingilia kati na kufika kushuhudia mradi wa lambo la maji uliogharimu zaidi ya milioni 511 uliojengwa na kampuni ya EDOS lakini zaidi ya miaka 10 wananchi hawapati maji.

Wakizungumza na Malunde 1 blog wananchi wamesema kuwa wanapata adha kubwa ya maji ambapo wakati wa kiangazi hununua ndoo moja kwa sh.300 lakini pia hata wagonjwa wanaopatiwa huduma ya afya katika kituo cha afya Magoto hupata shida ya maji na hivyo kulazimika kutoka na maji nyumbani kwao.

Maliam Nyeikobe mkazi wa kijiji cha Nyakonga ambaye pia ni mjumbe wa Serikali ya kijiji cha Nyakonga alisema kuwa Serikali ilitoa fedha kujenga Lambo la maji ili kumtua mama ndoo kichwani  lakini ni miaka kumi hawapati maji tangu lijengwe lambo hilo.

"Lambo lilijengwa kwa ajili ya kusambaza maji kwenye maeneo mbalimbali ya wananchi,kituo cha afya kinategemea maji ya kuvuna ya mvua yakikatika wananunua ndoo moja sh 300,ukienda kupata huduma kama kujifungua inabidi utoke na maji yako nyumbani ukafulie nguo", alisema Nyeikobe.

Elizabeth Ryoba alisema kuwa amechoka kufanya usafi na kulinda bomba kavu lisilotoa maji na kwamba wanateseka kupata huduma ya maji licha yakuwepo lambo la maji hivyo anaiomba Serikali kuwasaidia kupata maji kwakuwa walitoa maeneo yao kwa hiari kupitisha maji lakini hawajanufaika na mradi wa maji.

Joseph Gekobe alisema kuwa mradi wa Lambo ulianza kujengwa mwaka 2011 na kwamba sababu ya mabomba kutotoa maji ni kuwekwa kwa mipira ya kusambaza maji kutoka kwenye lambo la maji ambayo ni ya chini ya viwango.

"Mipira iloyowekwa ni miembamba sana na tanki la maji liko mlimani walipofungulia maji mipira ikashindwa kuhimiri kasi ya maji yote ikapasuka walifungulia siku moja ikapasuka yote maji yakashindwa kufika kwenye mabomba yaliyosambazwa kwa wananchi", alisema Gekobe.

Festo Gichonge alisema kuwa Lambo hilo lina maji lakini lipo kama pambo haruhusiwi mwananchi kuchota maji wala kunywesha mifugo na hivyo kuendelea kuteseka kutafuta maji kwenye visima vya asili.

Mnanka Robert alisema kuwa limejengwa chini ya kiwango na likakabidhiwa kinyemera kwenye kamati ya maji ya kijiji badala ya kukabidhi uongozi wa Serikali ya kijiji na wananchi

Getaro Gikaro ambaye pia ni mjumbe wa Serikali ya kijiji cha Nyakonga alisema kuwa baada ya mradi kukamilika ulipaswa kukabidhiwa kwa wananchi kwakuwa ni mradi wa wananchi ili nao waridhie kwakuwa umegharimu pesa nyingi za Serikali.

Zakaria Gikaro alisema kuwa wakati wa ujenzi Serikali ya kijiji haikushirikishwa katika hatua zote za ujenzi wa mradi zaidi tu ya kupewa taarifa ya ujenzi wa mradi.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mkuyuni Waitara Marwa kuliko lambo la maji alisema kuwa mipira ya kusambaza maji ilishindwa kuhimiri kasi ya maji yaliyokuwa yanatoka kwenye tenki kubwa la maji nakwamba wakati mradi unajengwa ilielezwa kuwa mradi huo utahudumia vijiji vinne.

Daud Chacha alisema : "jinsi lilivyochimbwa ni mbinu ya kujitengenezea fedha maana ni kwanini miradi mingine Serikali inafuatilia sana lakini huu mradi una zaidi ya miaka kumi hatupati maji lakini Serikali haijawahi kufatilia wala kuibana kampuni iliyojenga mradi na hata wakati wa kuchukua eneo la kujenga lambo wananchi walilipwa fidia kidogo ambao hawakuwa na maeneo wakalipwa fidia kubwa".

Mwenyekiti mstaafu Gabriel Matiko alisema kitendo cha kampuni kujenga mradi kwenye kijiji bila kushirikisha wananchi na uongozi wa Serikali ya kijiji ndiyo sababu ya miradi kujengwa chini ya viwango kwakuwa hakuna mtu wa kuwakagua au kuhoji.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Magoto Zabron Magabe alisema kuwa mradi huo ulikabidhiwa kwenye kamati ya maji ukiwa na mapungufu mengi.

"Hivi karibuni walifika watu wa maji wakasema wanakarabati Lambo cha hajabu wakatoa tope eneo dogo wakarundika udongo kandokando ya lambo bado tope zimo ndani tunaomba walete mabomba mapya waweke wasituwekee viraka",alisema Magabe.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyakonga John Ryoba alisema awali Lambo hilo lilikuwa linasimamiwa na idara ya maji halmashauri ya wilaya ya Tarime ambapo zaidi ya milioni 511 zilitumika na kwa sasa mradi huo unasimamiwa na Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) ambao nao unadaiwa  kutumia milioni 40 kati ya 75 kufanya ukarabati wa lambo.

"Hili lambo limejengwa chini ya kiwango mvua ikinyesha maji machafu yanatiririka kutoka mlimani yanaingia kwenye lambo,RUWASA walikuja wakasema wanakarabati lambo lakini walichokifanya ni kusafisha tu,hata kingo zilizowekwa kuzuia maji kupita zimepangwa tu mawe ambayo hayajachapiwa kwa saruji na pengine wametumia saruji kidogo kuta zinabomoka", alisema.

"Waziri mkuu Majaliwa katika Ziara yake Tarime wakati anapita Nyakonga wananchi walijiandaa kusimamisha msafara wake ili wamweleze kero zao wakiwa na mabango ya kumwonyesha kuhusu lambo la maji lakini tukazuiwa tumuoneshe mabango Waziri akapita wananchi tukanyimwa haki ya kueleza matatizo yao",alisema Ryoba.

Ryoba aliiomba Serikali kuingilia kati huku akimuomba Rais Magufuli kuwasaidia ili waweze kupata maji kwa kuwa mradi huo umetumia fedha nyingi za Serikali jambo ambalo wananchi wanashangaa kuona hatua hazichukuliwi kuhakikisha wanapata huduma ya maji.


Mwenyekiti wa kijiji cha Nyakonga akionyesha maji yanavyotiririka kuingia kwenye lambo la maji
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post