DC MBONEKO AGEUKA MBOGO WAFANYAKAZI MGODI WA DHAHABU MAHIGA - MWAKITOLYO KUNYANYASWA NA WAWEKEZAJI

 

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akizungumza na wafanyakazi wa Mgodi wa madini ya Dhahabu (ZEMD) uliopo Mahinga- Mwakitolyo wilayani humo, unaomilikiwa na Raia wa China, wakati akisikiliza na kutatua kero zao.

Na Marco Maduhu, Shinyanga. 
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, amefanya ziara ya kusikiliza na kutatua kero za wafanyakazi katika mgodi wa madini ya Dhahabu (ZEMD) uliopo Mahiga Kata ya Mwakitolyo wilayani humo, ambao unamilikiwa na Raia wa China.

Ziara hiyo imefanyika Januari 26,2021 ambapo mkuu huyo wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, aliambatana na kamati ya ulinzi na usalama wilaya, wataalamu wa madini, Afisa kazi, wakala wa usalama na afya mahala pa kazi OSHA pamoja na Afisa kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC). 

Akizungumza mara baada ya kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi wa mgodi huo, Mboneko amesikitishwa na manyanyaso ambayo wanafanyiwa na waajiri wao, likiwemo suala la kutothaminiwa uhai wao, kutumikishwa muda mrefu bila ya kupewa chakula, mikataba mibovu, kutopewa vifaa kinga, pamoja na kufukuzwa hovyo bila ya utaratibu hasa pale wanapoumia. 

Aidha akitoa maagizo kwa uongozi wa mgodi huo, amewataka wabadili mienendo yao na kuacha kunyanyasa wafanyakazi wao, bali wafuate sheria za nchi, ajira, masuala ya usalama na afya kazini, utunzaji wa mazingira, pamoja na kuacha kuwapiga na kuwatolea lugha za matusi. 

"Serikali tunahitaji sana wawekezaji, lakini mfuate sheria za nchi na taratibu zote zilizowekwa, na siyo kunyanyasa wafanyakazi ambao ni Watanzania, na leo nimekuja ili kuwekana sawa,kwa sababu kama hakuna amani kwenye mgodi huu, basi haina haja ya nyie wawekezaji kuwepo hapa," amesema Mboneko. 

"Nafahamu Tanzania na nchi ya China sisi ni marafiki, lakini nyie mnachokifanya hapa kwa wafanyakazi wenu si sahihi kabisa. Fanyeni kazi katika mazingira rafiki, ili na hawa watumishi wenu licha ya kupata ajira nao wafurahie kazi yao na siyo kuwanyanyasa," ameongeza. 

Pia ametoa mwezi mmoja kwa uongozi wa mgodi huo, mapungufu yote ambayo yamejitokeza wayafanyie kazi, pamoja na Wakala wa usalama na afya kazini OSHA, na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), watembelee kumaliza changamoto zote mgodini hapo, ili kuhakikisha usalama wa wafanyakazi una kuwapo. 

Katika hatua nyingine aliutaka mgodi huo kuajiri mtu ambaye atakuwa akisikiliza kero za wafanyakazi, meneja rasilimali watu (HR), na kisha kuziwasilisha kwa viongozi wa mgodi na kutafutiwa ufumbuzi, kuliko hivi sasa wanaisha bila ya kuwapo kwa mtumishi huyo wa kuwasemea shida zao. 

Nao baadhi ya wafanyakazi wa mgodi huo, awali wakiwasilisha kero zao kwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, wamesema kwenye mgodi huo hawana mikataba ya ajira ambayo ni halali, na wamekuwa wakisainishwa bila ya kuusoma na wala hawajui kiwango cha mshahara. 

Aidha wamesema wamekuwa wakikatwa makato ya NSSF, pamoja na Kodi inayofahamika Magufuli, bila ya kupewa risiti, na wala kutokuwa na namba ya makato ya NSSF, huku wakikatwa kiwango cha fedha kisichokuwa na kiwango sahihi. 

Pia walilalamikia suala la usalama kazini ,ambapo wanafanya kazi bila ya kupewa vifaa kinga, pamoja na kulazimishwa kufanya kazi kwenye maeneo ambayo yana moshi wa sumu (blasting), na wakigoma kufanya kazi hadi moshi huishe hutishiwa kufukuzwa kazi ama kufukuzwa kabisa. 

Mmoja wa wafanyakazi hao Yohana Daudi, amesema Wachina wamekuwa wakilipua miamba(blasting) kipindi wao wapo chini ya shimo, ambapo moshi wa sumu huwa unawazidi, na kusababisha baadhi yao kuzimia, na wanapotoka nje hufokewa na kulazimishwa warudi tena shimoni. 

"Juzi tu kidogo watu tufe kwa kosa hewa, mara baada ya Wachina kulipua miamba( blasting) ambapo Moshi wenye sumu ulituzidi na wenzangu wawili waliishiwa nguvu na kuzimia, ikabidi niwapandishe kwenye vibelenge kinyume na utaratibu ndipo tukatoka nje, lakini ukiwazuia wasifanye hivyo sisi tunapokuwa chini hawaelewi," amesema Daudi. 

Naye Teddy Malima ,ambaye ni mtaalamu wa kutengeneza Baruti, alilalamikia suala la kutopewa vifaa kinga ,zikiwamo groves, pamoja na Masks, huku pia wakiwa wanapewa kazi zingine ambazo siyo taaluma zao. 

Kwa upande wake Kaimu meneja wakala wa usalama na afya mahali pa kazi (OSHA) Kanda ya ziwa Mhandisi Mjawa Shenduli, amesema awali walishatoa maelekezo kwenye mgodi huo juu ya kufuata sheria za usalama na afya, lakini bado hawazingatii, na kubainisha hatua inayofuata ni kuwapiga faini. 

Aidha Meneja msaidizi wa mgodi huo wa (ZEMD) Zhao Chao, amesema watarekebisha makosa yote ambayo wamepewa maelekezo na Serikali, ili kuhakikisha changamoto zote zinatatuliwa, na wafanyakazi wao kufanya kazi kwa Uhuru na kupata stahiki zao kwa mujibu wa sheria, ikiwamo na mikataba halali inayoonyesha kiwango cha mishahara yao.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akizungumza na wafanyakazi wa Mgodi wa madini ya Dhahabu (ZEMD) uliopo Mahinga- Mwakitolyo wilayani humo, wakati akisikiliza na kutatua kero zao.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akiendelea kutoa maelekezo ya Serikali, wakati akitatua kero za wafanyakazi kwenye Mgodi wa dhahabu (ZEMD)uliopo Mahiga Kata ya Mwakitolyo wilayani humo, ambao unamilikiwa na Raia wa China.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akiendelea kusisitiza jambo kwenye kikao hicho.
Afisa kazi mkoani Shinyanga Revocatus Mabula, akitoa maelezo namna ya kuajiri wafanyakazi na kupata stahiki zao.
Kaimu meneja wakala wa usalama na afya mahali pa kazi (OSHA) Kanda ya ziwa Mhandisi Mjawa Shenduli, akielezea jinsi maelekezo ya usalama na afya ambayo walishayatoa awali kwenye mgodi huo.
Mhandisi Mchenjuaji kutoka Ofisi ya madini mkoani Shinyanga Camilius Seneda, akizungumza kwenye kikao hicho cha utatuzi wa kero za wafanyakazi wa mgodi wa ZEMD.
Afisa kutoka ofisi ya uhamiaji mkoani Shinyanga Godson Mwanawima, akizungumza kwenye kikao hicho cha utatuzi wa kero za wafanyakazi katika Mgodi wa ZEMD.
Awali katibu tawala wilaya ya Shinyanga Boniphace Chambi, akifungua kikao hicho cha utatuzi wa kero za wafanyakazi katika mgodi wa ZEMD.
Mfanyakazi wa Mgodi wa ZEMD Philibert Elisha akitoa kero kwenye kikao hicho.
Mfanyakazi wa Mgodi wa ZEMD Juma Gambaliko, akitoa kero kwenye kikao hicho.
Mfanyakazi wa Mgodi wa ZEMD Yohana Daudi, akitoa kero kwenye kikao hicho.
Mfanyakazi wa Mgodi wa ZEMD Teddy Malima akitoa kero kwenye kikao hicho.
Meneja msaidizi wa mgodi huo wa (ZEMD) Zhao Chao, akitoa majibu ya utekelezaji wa maagizo ya Serikali kutoka kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko.
Watumishi wa Mgodi wa ZEMD wakiwa kwenye kikao cha usikilizwaji wa kero zao na kutafutiwa ufumbuzi.
Watumishi wa Mgodi wa ZEMD wakiwa kwenye kikao cha usikilizwaji wa kero zao na kutafutiwa ufumbuzi.

Watumishi wa Mgodi wa ZEMD wakiwa kwenye kikao cha usikilizwaji wa kero zao na kutafutiwa ufumbuzi.
Kikao cha usikilizwaji wa kero na utatuzi kikiendelea.
Kikao cha usikilizwaji wa kero na utatuzi kikiendelea.
Kikao cha usikilizwaji wa kero na utatuzi kikiendelea.
Kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Shinyanga ikiwa kwenye kikao hicho.
Awali mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akiwasili kwenye Mgodi wa ZEMD kwa ajili ya kusikiliza kero za wafanyakazi wa Mgodi huo na kuzitafutia ufumbuzi. akimpokea na Meneja Msaidizi wa mgodi huo Zhao Chao.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, mara baada ya kumaliza kusikiliza kero za wafanyakazi wa Mgodi wa ZEMD na kuzitafutia ufumbuzi, alikwenda pia kuangalia ujenzi wa kituo cha Polisi Mwakitolyo.

Na Marco Maduhu- Shinyanga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post