BENARD MEMBE AIPIGA CHINI ACT WAZALENDO



Aliyekuwa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo na mshauri wa Chama hicho, Bernad Membe leo Januari 1,2021 ametangaza rasmi kujiuzulu nafasi zake zote ndani ya chama hicho akisema hakulazimishwa na mtu yoyote baloi ni uamuzi wake binafsi. 

Membe aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania kati ya 2007 hadi 2015 ametangaza uamuzi huo leo akiwa nyumbani kwake kijijini Rondo Chiponda, Wilaya ya Mtama Mkoani Lindi ambapo amesema hajafanya uamuzi huo kwa shinikizo lolote na kwamba kwa sasa atakuwa mshauri wa masuala mbalimbali yanayoihusu nchi ya Tanzania na kupigania demokrasia ya kweli.


“Wiki tatu zilizopita nilitangaza kwamba ifikapo Januari Mosi, 2021 nitajiuzulu nafasi yangu ya ushauri mkuu wa ACT-Wazalando na uanachama wa chama hicho kwa mpigo.

“Ninatumia haki yangu ya kikatiba kujiuzulu kwenye nafasi yangu ya ushauri mkuu ya chama na uanachama wa ACT-Wazalendo kwa hiari yangu mwenyewe bila kulazimishwa wala kutishiwa na mtu yeyote na bila kuadhirika na jambo lolote.

“Ibara ya 105 kifungu kidogo cha kwanza kinasema mwanachama atakoma kuwa mwanachama na atajiuzulu iwapo atatangaza hadharani kwamba anajiuzuli au ataandika barua kwa viongozi wa chama na mimi nimefanya yote mawili nimeshamuandikia barua zitto Kabwe ili aweze kupata uamuzi wangu, hivyo kuanzia sasa mimi si mwanachama wa ACT Wazalendo,” amesema Membe.

Mwanadiplomasia huyo alitangaza kujiunga na Chama cha ACT Wazalendo Julai, 2020 miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2020 baada ya kufukuzwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tarehe 28 Februari 2020 na Kamati Kuu ya chama hicho, kisha uamuzi huo kubarikiwa na Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), tarehe 10 Julai 2020.

Membe alifukuzwa kwa tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya CCM, pamoja na kuonywa mara kadhaa, pasina kubadilika.

Baada ya kuhamia ACT Wazalengo, Membe alitangaza kugombea kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho.

Akijiunga ACT Wazalengo Membe alisema ; “Kwa hiari yangu nimeamua kujiunga katika familia kubwa ya ACT Wazalendo inayotaka mabadiliko yenye lengo la kuwanufaisha Watanzania wengi hasa wakulima, wafanyabiashara, watumishi wa serikali, wafanyakazi mbalimbali na wote wanaoitakia kheri Tanzania yetu. Nataka kupigania mabadiliko ya kweli ya hii nchi kupitia ACT na azma yangu itatimia".

Hata hivyo kuliibuka migogoro ndani ya chama hicho baada ya Viongozi wa ACT Kutangaza kumuunga mkono Mgombea Urais kupitia CHADEMA, Tundu Lissu licha ya Membe kuwa mgombea Urais kupitia ACT Wazalendo ambapo alianza kutofautiana na viongozi wenzake baada ya kusitisha kampeni za urais.

Ijumaa Oktoba 16, 2020 Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe alitangaza kumpigia kura mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni mjini Kigoma.

Mbali na Zitto, Mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad aliwahi kutangaza kuwa chama hicho kitamuunga mkono Lissu katika Urais ambapo pia Lissu pia aliwahi kutangaza kuwa Chadema itamuunga mkono Maalim Seif katika urais wa Zanzibar.

Hata hivyo Membe alisisitiza kuwa yeye ni mgombea halali wa Urais kupitia ACT Wazalendo.

“Mimi Bernard Membe ni mgombea halali wa ACT-Wazalendo wa nafasi ya Urais. Na chama chetu ni kizuri kabisa ambacho nitakipeleka 28 Oktoba 2020 vizuri kabisa”,alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post