BABA AUA MTOTO WAKE KWA KUMVUNJA SHINGO NA UTI WA MGONGO


Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi
***
Jeshi la polisi mkoani Kagera, linamshikilia Amos Rudovick (39) kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mtoto wake Dastan Amos (13), kwa kumchapa na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na baada ya uchunguzi ilibainika kuwa alimvunja shingo na uti wa mgongo.

Kamanda wa polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi, amesema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 02, 2021, katika kijiji cha Ibale wilayani Kyerwa, baada ya mtoto huyo ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Ibale, kuondoka nyumbani kwao kwenda kutembea bila idhini ya wazazi na kurejea nyumba saa 9:00 Alasiri.

"Baba yake alimuadhibu kwa kumchapa bila huruma maeneo mbalimbali ya mwili wake kwa kutumia fimbo yenye unene mkubwa, uchunguzi wa kitabibu umefanyika na kubainika kwamba marehemu alikutwa amevunjwa shingo pamoja na uti wa mgongo na ndicho kimethibitishwa kuwa ndiyo chanzo cha kifo cha huyo mwanafunzi", amesema Kamanda Malimi.

Aidha kamanda huyo amesema kuwa jeshi hilo linaendelea kuchunguza tukio la mama mmoja Jesca Samson, mwenye umri wa miaka 37, aliyefariki dunia kwa kunywa sumu ya panya na kumnywesha mtoto wake wa kiume Jordan Samson, mwenye umri wa miaka mitatu ambaye amenusurika kifo baada ya kukimbizwa hospitali.

"Mama huyo alikunywa sumu usiku wa kuamkia Januari 01, 2021, wakati huo mume wake ndipo alikuwa amerejea nyumbani Desemba 31, 2020 baada ya kuachiwa kutoka gerezani alikokaa kwa muda wa miezi mitatu kutokana na kesi hiyo ya kuuza ardhi", amesema.

CHANZO - EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post