RAIS MAGUFULI KUWEKA JIWE LA MSINGI JENGO LA OPD HOSPITALI YA MJI KAHAMA, KUZINDUA MRADI WA MAJI

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack akizungumza na waandishi wa habari wilayani Kahama
Na Salvatory Ntandu - Kahama
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli anatarajia kuanza ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo ambapo ataweka mawe ya msingi katika majengo mbalimbali pamoja na kuzindua mradi wa maji wa Kagongwa - Isaka.

Akizungumza leo Jumanne Januari 26, 2021 na Waandishi wa habari wilayani Kahama,Telack amesema kuwa Rais Magufuli ataweka jiwe la msingi la wagonjwa wa nje hospitali ya Kahama Mji ambalo limegharimu shilingi bilioni 3.9 fedha za mapato ya ndani kwa lengo la kupunguza msongamano kwa akina mama wanaokwenda kujifungua katika hospitali hiyo Januari 28,2021.

Alisema kuwa kwa siku katika hospitali ya Mji Kahama zaidi ya watoto wachanga 35 hadi 75 wanazaliwa hivyo kusababisha akina mama wajawazito kukosa sehemu salama ya kujifungulia kutokana na kupokea idadi kubwa ya wajawazito kwa siku.

“Kwa mwezi watoto wapya zaidi 1000 wanazaliwa katika hospitali hii,serikali imejenga jengo hili la ghorofa mmoja ambalo litakuwa maalumu kwaajili ya kinamama wajawazito na watoto,tumetumia shilingi milioni 204 kujenga kituo cha afya Maalumu cha Nyasubi ambacho ni mahususi pia kwa akinamama kujifungulia,”alisema Telack.

Telack amefafanua kuwa bado akina mama wajawazito wanakabiliwa na changamoto mbalimbali lakini kukamilika kwa jengo hilo litasaidia kupunguza msongamano wa akinamama wajawazito katika hospitali hiyo ambayo inapokea idadi kubwa ya wagonjwa kwa siku huku wengi wao wakiwa ni akinamama wajawazito.

Amefafanua kuwa Januari 29,2021 pia Rais Dk Magufuli ataweka jiwe la msingi katika jengo la utawala la halmashauri ya Mji kahama na Viwanda vya mwekezaji Mzawa vya Kampuni ya KOM GROUP OF CAMPANIES vya kusindika mazao mbalimbali ambacho kinatarajiwa kutoa ajira mpya kwa wakazi zaidi ya 2000.

“Pia Rais Magufuli atazindua mradi mkubwa wa maji ya ziwa Viktoria wa Kagongwa –Isaka ambao umekamilika na wananchi wameanza kupata huduma,niwaombe wakazi wa mkoa huu kujitokeza kwa wingi kumsikiliza katika mitutano yake miwili anatakayowahutubia,”alisema Telack.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post