Breaking : RAIS MAGUFULI AIPANDISHA HADHI KAHAMA MJI KUWA MANISPAA YA KAHAMA...AMSAMEHE MKURUGENZI ALIYEJINUNULIA SHANGINGI KALI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa Chapulwa Kahama mara baada ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa Kiwanda cha Nafaka, Vinywaji na Maziwa (Kom Limited) Kahama mkoani Shinyanga leo tarehe 28 Januari 2021. Picha na Ikulu
Viongozi mbalimbali pamoja na wabunge wakipiga makofi mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kutangaza kumsamehe Mkurugenzi wa Halmashauri ya  Mji wa Kahama Anderson David Msumba (aliyesimama) ambaye alikuwa miongoni mwa Wakurugenzi wachache walionunua Magari ya Kifahari tofauti na maagizo ya Serikali.
***

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ameipandisha hadhi halmashauri ya Wilaya ya Kahama Mji kuwa Manispaa ambapo sasa Kahama Mji itajulikana kama Manispaa ya Kahama akisema  wilaya hiyo imemfurahisha kwa kuwa na mipango mikubwa anayoitaka ikiwa ni pamoja na kufanya kazi nzuri ya ukusanyaji wa mapato na kutekeleza miradi yake ya maendeleo kwa fedha zake za ndani.

Rais Magufuli amesema hayo leo Alhamis Januari 28,2021 wakati akizungumza na wananchi katika uwanja wa taifa wilayani Kahama mkoani Shinyanga ambapo wananchi waliokuwa katika mkutano huo walishangilia kutokana na tangazo hilo.

“Nimeshangaa kweli, kwamba wilaya hii ya Kahama ina mipango mikubwa ninayoipenda. Na mimi nasema kwa sababu mmenipa kura halafu mimi ndiyo Rais na kazi ya kupandisha ninyi mmenipa, ninaipandisha iwe manispaa, na hiyo hospitali ya Kahama iwe na hadhi ya Manispaa  na nitahakikisha mji wa Kahama unajengewa barabara za lami ili ziendane na hadhi ya manispaa”, amesema Rais Magufuli.

“Nina sababu za msingi za kuipandisha, kwanza mapato ya wilaya ya Kahama  katika mkoa mzima wanachangia asilimia 50, hata makusanyo ya mapato ni miongoni mwa halmashauri zinazoongoza kwa makusanyo. Hata kura mlinipa kwa wingi, hata katika miradi ninyi mnajitegemea,” amesema Rais Magufuli.

“Najua kule Shinyanga hawana raha, lakini kikubwa mimi ninataka maendeleo na watu wanaoamua kutengeneza maendeleo yao, mimi lazima niwaunge mkono. kwa hiyo Kahama mmenigusa sana”,ameongeza.

Mkoa wa Shinyanga sasa utakuwa na Manispaa mbili (Manispaa ya Shinyanga na Manispaa ya Kahama), lakini pia kuwa na halmashauri za wilaya nne ambazo ni halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Shinyanga, Ushetu na Msalala.

Rais Magufuli pia amemsamehe Mkurugenzi wa Kahama Mji, Anderson Msumba ambaye ni miongoni mwa wakurugenzi wachache waliokuwa na kashfa kwa kununua magari ya kifahari tofauti na maagizo ya serikali ambapo amesema amemsamehe na kumuachia gari hilo kutokana na jinsi anavyofanya kazi vizuri na kwa kujituma akishirikiana na madiwani ambapo wamekuwa wakitekeleza miradi yenye kuwaletea maendeleo wananchi.

“Nilianza kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi ya Halamshauri ya Wilaya utakaogharimu Sh1.8 bilioni. Nilipata bahati ya kupata maelezo ya wahandisi akina mama waliojenga. Kilichonifurahisha zaidi, ofisi ile inajengwa kutokana na mapato ya ndani ya Halmashauri,” amesema Rais Magufuli.

“Nikaambiwa jengo hilo limejengwa kwa mapato ya ndani aya halmashauri hii. Nikawa namwangalia mkurugenzi, alikuwa na ka- tuhuma kidogo ka - kujinunulia gari, nikasema kama fedha na kupitia madiwani wamejenga hili jengo la Sh1.8 bilioni, wanajenga jengo la hospitali kubwa tu la Sh 3.2 bilioni, ngoja nione mpaka mwisho.

“Nikaenda kwenye kiwanda, nikaona ni maviwanda yale yale niliyoyaona Ulaya. Nasema kwa dhati kwa sababu viwanda vinavyojengwa Ulaya ni hivyohivyo. Nilipopewa taarifa pale, nikaambiwa ardhi hii yote ilitolewa na halmashauri ni ekari 90 bure. Nikajiuliza sana. Nataka niwaambie ndugu zangu kwamba huyu mkurugenzi na madiwani wana akili sana,” amesema Rais Magufuli.

"Mkurugenzi wa Kahama Mji unafanya kazi kubwa sana, ka kosa kale kadogo kamesamehe dhambi zako zote. Najua unapigwa vita, ila wanaokupiga vita kuanzia sasa wakuogope.

 "Kahama panapendeza, Huyu Mkurugenzi wa Kahama ana akili sana, alikuwa na makosa ya kujinunulia gari. Lakini leo nimekusamehe na gari nakurudishia ufanye kazi zako ila usijinunulie tena gari kinyume na utaratibu. Nimemsamehe Mkurugenzi huyu, amefanya makubwa! Mkurugenzi hongera Sana",amesema Magufuli.

"Mkurugenzi wa Kahama na Madiwani wana akili sana, wametoa eneo bure hawakumuuzia Muwekezaji, wameangalia mbele kwamba watatengeneza ajira na wataongeza kodi, ni busara kubwa sana",ameongeza Rais Magufuli.

Rais Magufuli pia amemuagiza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Doroth Gwajima kuipandisha hadhi hospitali ya Mji Kahama iendane na hadhi ya Manispaa.

"Nawaongezea Sh Milioni 500 kuchangia jengo la hospitali ya mji Kahama. Na kwa vile waziri wa afya yuko hapa aipandishe hadhi hiyo hospitali ili endane na hatua ya Manispaa," amesema Rais Magufuli.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments