WATENDAJI WATAKIWA KUWA NA IDADI KAMILI YA WANAFUNZI WALEMAVU NA WANAOPATIWA MSAADA


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka maafisa Ustawi wa Jamii Mkoani humo kuainisha idadi kamili ya wananfunzi wenye ulemavu wa aina mbalimbali katika shule za Msingi na Sekondari na namna wanavyosaidiwa katika kusaidiwa kupata elimu kulingana na mazingira yao.

Mh. Wangabo amesema kuwa kwa muda mrefu serikali imekuwa ikiwahamasisha wazazi kutowaficha watoto wenye ulemavu kwa kuwapeleka shule lakini takwimu za kimsaada kwa Watoto hao hazijulikani kwa wazazi wengine ambao bado wanawaficha Watoto wao wakidhani kuwa hawapatiwi msaada stahiki.

“Kwasababu akimpeleka shule kuna changamoto kubwa, kuna mwenye ulemavu wa viungo lakini hana vifaa saidizi atafanyaje? Lakini tukijielekeza kuwasaidia hawa ambao wako mashuleni basi na wale ambao wako majumbani watahamasika sasa kuwapeleka shuleni kwasababu tayari sasa wana vifaa saidizi, wanaona kabisa jamii inawajali, mashirika makampuni yanawajali, kwahiyo wakati tunasema Watoto wenye ulemavu wasifichwe watolewe waende shule basin a wale waliopo shule tuwafahamu, tuwasadidie ili na wale wengine waweze kuona jamii sasa inawajali,” Alisisitiza.

Mh. Wangabo ameyasema hayo katika hafla fupi ya kukabidhi vifaa saidizi kwa viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Pamoja na Chama cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) vilivyotolewa na Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC PLC).

Wakati akitoa taarifa fupi ya hali ya watu wenye ulemavu mkoani humo Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Rukwa Godfrey Mapunda alisema kuwa kuanzia mwaka 2019 hadi 2020 mkoa umetambua jumla ya watu wenye ulemavu 1,616 ambao kati ya hao wenye umri chini ya miaka 18 ni 574 na wenye umri wa Zaidi ya miaka 18 ni 1,042 huku wanaume wakiwa 923 na wanawake 693.

Kwa upande wake mwakilishi wa Kampuni ya Sigara Tanzania Oscar Lwoga alisema kuwa kampuni hiyo imewasilisha baiskeli za miguu mitatu 10, fimbo nyeupe 61 na magongo 74 kwaajili ya kusaidia sehemu ndogo ya wahitaji wa vifaa hivyo saidizi katika mkoa wa Rukwa.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post