DKT. KALEMANI AELEKEZA TANESCO KUKATA UMEME KWA WADAIWA WOTE


 Na Eliud Rwechungura
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesisitiza Kazi, Ubunifu na Usahihi kwa watumbishi wa wizara hiyo huku akiiagiza TANESCO kukata umeme kwa wadaiwa wote nchi nzima.

Dkt. Kalemani ameyasema hayo  Desemba 12, 2020 katika kikao kazi cha kwanza kilichojumuisha Wakuu wa Bodi, Menejimenti, Idara, Vitengo na Taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo kilichofanyika katika ofisi za wizara zilizopo Mji wa kiserikali Mtumba Dodoma kilichokuwa na lengo la kufahamiana na kutoa maagizo na maelekezo mbalimbali ya msingi ambayo yanapaswa kutekelezwa katika Serikali ya awamu hii.

“Nimewaita kwa mambo mawili tu, jambo la kwanza ni kufahamiana ndilo jambo lililonifanya niwaite wajumbe wa bodi zote za wakurugezi na menejimenti pamoja na uongozi wa wizara na kufahamishana mambo ya msingi ya kufanyia kazi na jambo la pili ni kuwaarifu kuwa tumeanza kufanya kazi na kikao hiki sio kikao tu bali ni kikao cha kwanza cha kazi”

Dkt. Kalemani ameanza kwa kusisitiza kauli mbiu itakayotumika kwa kipindi hiki cha miaka mitano ambayo ni Kasi, Ubunifu na Usahihi na amezidi kuwataka watumishi wote Wizara hiyo kufanya kazi kwa kasi kubwa huku wakizingatia ubunifu na kwa usahihi wa kazi huku akiasa kila mtumishi kutimiza wajibu wake na akaendelea kutoa rai ya kupambana na mtu ambaye hatatimiza wajibu wake katika kazi.

“Nitangulie kusema tunakwenda na kauli mbiu ifuatayo, ndiyo kauli mbiu yetu kwa miaka hii mitano ya kipindi cha pili cha awamu ya tano. Kauli mbiu yetu ni Kasi, Ubunifu na Usahihi, kila mmoja atakachoelezwa hapa akifanye kwa kasi kubwa, Ubunifu na Usahihi”

Dkt. Kalemani ameagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wahakikishe wanatekeleza majukumu yao yote kwa ufasaha huku akiiagiza wakurugezi wote wa Shirika hilo nchi nzima kuendelea kushugulikia na kutatua kero mbalimbali kama kukatika kwa umeme mara kwa mara na kero nyingine pia kuhakikisha miradi yote inayosimamiwa na Shirika hilo inatekelezwa kwa wakati.

Aidha, Dkt. Kalemani ameendelea kutoa maagizo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) la kukata umeme kwa wadaiwa wote nchi nzima bila kujali Taasisi binafsi wala Taasisi za umma huku akiwataka wakurungezi wote kuhakikisha wanakusanya mapato kutoka kwa wateja wao

“Lazima TANESCO tukusanye mapato kutoka kwa wateja wetu maana jana nilipoingia ofisi nimepokea taarifa mpaka sasa tunadai zaidi ya Bilioni 182 kwa Taasisi za umma na wateja wa kawaida Bilioni 3.6, Mwenyekiti wa bodi nakuagiza kwa tunaemdai kata umeme, acha nilaumiwe mimi kwanza, kwahiyo kuanzia leo kama kuna mteja au Taasisi iwe ya Umma au ya binafsi tunayoidai naelekeza kwa bodi ya TANESCO katieni umeme kuanzia leo”

Nae Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato ameendelea kusisitiza watumishi wote wa Wizara hiyo kutimiza wajibu wake huku akiwasihi kutekeleza kikamilifu maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri na yatakayoendelea kutolewa na viongozi wa Wizara hiyo na Serikali nzima kwa ujumla.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments